• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
WALIOBOBEA: Obure: Moi, Kibaki na Uhuru walimwaminia

WALIOBOBEA: Obure: Moi, Kibaki na Uhuru walimwaminia

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

KAMA sehemu ya mazungumzo ya kukomesha ghasia zilizozuka nchini baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, serikali ya Muungano wa Kitaifa iliundwa Mwai Kibaki akiwa Rais na Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu.

Viongozi hao wawili waliunda Baraza la Mawaziri 40 ambalo Christopher Mogere Obure aliteuliwa Waziri wa Ujenzi.

Huo haukuwa wadhifa wa kwanza wa Obure serikalini, alikuwa waziri mwenye nguvu katika utawala wa Rais Daniel arap Moi, aliyemteua waziri wa Fedha kuchukua nafasi iliyoachwa na Chris Okemo kufuatia malalamishi kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.

Wakati huo, BBC iliripoti kwamba mabadiliko ya baraza la mawaziri lilikuwa “jaribio la Rais Moi kupata mawaziri zaidi wanadiplomasia kuongoza mashauriano na Benki ya Dunia na IMF (Shirika la Fedha Ulimwenguni) katika juhudi za kuyashawishi kuachilia pesa ambazo yalikuwa yamezuia”.

Katika mageuzi hayo, aliyekuwa rais wa nne wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliteuliwa waziri kwa mara ya kwanza.

Katika serikali ya Kenyatta, Obure alikuwa waziri msaidizi katika Wizara ya Uchukuzi na Miundomsingi.

Akiwa waziri wa ujenzi wa umma, anatambuliwa kwa kukabiliana na wanakandarasi wasiohitimu na kuinua wizara hiyo baada ya miaka mingi ya kuporomoka kutokana na ufisadi, wahudumu matapeli, uwezo duni, ukosefu wa pesa za kutosha na upuuzaji wa sheria.

Obure alitetea kuundwa kwa Mamlaka ya Taifa ya Ujenzi (NCA) kupitia Mswada wa Mamlaka ya Taifa ya Ujenzi 2011 ambao ulipatia NCA nguvu za kuwapiga marufuku wanakandarasi walaghai ambao awali walikuwa wakisababishia serikali hasara ya mabilioni ya pesa.

Obure alijiunga na serikali kwa mara ya kwanza mwaka wa 1984, akiwa Waziri Msaidizi wa Leba chini ya marehemu Robert Ouko.

Alichaguliwa bungeni kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi mkuu wa 1983 kuwakilisha eneobunge la Machoge-Bassi.

Obure alikuwa amegombea kiti hicho mwaka wa 1969, lakini akashindwa na Zephania Mogunde Anyieni. Aligombea tena kwenye uchaguzi mkuu wa 1979 na kuibuka wa pili.

Baadaye Machoge-Bassi iligawanywa kuunda maeneo bunge ya Bomachoge na Bobasi mwaka wa 1988 na Obure akawa mbunge wa kwanza wa Bobasi.

Katika uchaguzi mkuu wa 1992 alishindwa na Bw Stephen Manoti.

Alishinda uchaguzi mkuu wa 1997 na kuteuliwa waziri msaidizi wa uchukuzi na mawasiliano. Nyachae alipojiuzulu baada ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Fedha hadi wizara ya viwanda, Moi alimteua Obure waziri wa viwanda.

Mwaka wa 2000, alihamishiwa wizara ya vyama vya ushirika. Wakati Moi alipopunguza wizara hadi 15, Obure aliteuliwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mwaka wa 2001, Moi alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kumhamishia Obure wizara Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa, ambako alihudumu kwa chini ya mwaka mmoja kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Fedha.

Obure aliposhindwa na Manoti katika uchaguzi mkuu wa 2002, alibaki katika baridi kisiasa hadi 2007 aliposhinda kwa tiketi ya chama cha Orange Democratic Movement.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, wa kwanza chini ya katiba mpya, Obure aliamua kugombea kiti cha useneta kaunti ya Kisii na kuwa seneta wa kwanza wa kaunti hiyo.

  • Tags

You can share this post!

DARUBINI YA WIKI, Toleo Nambari 10, Novemba 06, 2022

KIGODA CHA PWANI: Madeni, ufisadi vyadumaza ukuaji wa...

T L