• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
WALIOBOBEA: Parpai aliangusha mbabe, akawa waziri miezi 7 tu

WALIOBOBEA: Parpai aliangusha mbabe, akawa waziri miezi 7 tu

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

GEOFFREY Mapukori Parpai ni waziri aliyehudumu kwa muda mfupi, wa miezi saba, katika Baraza la Mawaziri la Rais Mwai Kibaki.

Kwa hivyo, ni vigumu kupima kazi yake kama waziri, kwa kuwa aliugua muda mfupi baada ya kuteuliwa waziri aliyesimamia wafanyakazi.

Kisiasa, Parpai alikuwa mwanachama shupavu wa chama cha Democratic Party of Kenya (DP) kilichoanzishwa na Kibaki tangu alipogombea kiti cha ubunge cha Kajiado Kusini mwaka wa 1992 na kushindwa na Philip Lampat Sing’aru wa chama cha Kenya African National Union (KANU).

Sing’aru alikuwa ameshinda kiti cha Kajiado Kusini kwenye uchaguzi uliokosolewa mno wa mlolongo mwaka wa 1988 – ingawa pia alisaidia kuunda maisha ya kisiasa ya Kibaki katika Kanu ambacho kilikuwa chama tawala wakati huo.

Wakati huo Parpai aliyekuwa na umri wa miaka 35, alikuwa akifanya kazi ya ukarani katika Baraza la Mji wa Olkejuado. Ili kujiunga na siasa za Kajiado, hakuwa na budi kujihusisha na watu waliokuwa maarufu katika wilaya hiyo.

Ujio wa vyama vingi vya kisiasa mwaka wa 1991 baada ya kuondolewa kwa Sehemu ya 2A ya Katiba ya Kenya, iliyokuwa imeruhusu Kanu kutawala siasa za kitaifa Kenya, Parpai alihamia DP ambacho Kibaki aliunda 1991 akiwa na John Keen, mmoja wa mibabe wa siasa wakati huo katika Kaunti ya Kajiado.

Kibaki aliunda DP kuwa chama cha kuhifadhi wanasiasa wasiokuwa na misimamo mikali ambao hawangetoshea katika chama cha Forum for the Restoration of Democracy (FORD) kilichokuwa na wanasiasa kama Jaramogi Oginga Odinga na akapewa heshima katika chama hicho.

Kwa hivyo, uchaguzi wa 1992 Kajiado ulihusisha mibabe Keen wa DP ( Kajiado Kaskazini) na Parpai (Kajiado Kusini) dhidi ya wagombeaji wa Kanu, George Saitoti (Kajiado Kaskazini) na Sing’aru (Kajiado Kusini).

Kwa ubabe ulioshangaza, Parpai alizoa kura 9,383 dhidi ya 12,292 za Sing’aru. Katika eneobunge jirani la Kajiado Kaskazini, Saitoti alipata kura 18,940 dhidi ya 8,242 za Keen.

Matokeo haya yalionyesha kuwa chama cha DP cha Kibaki kilikuwa kimepenya katika ngome ya Wamaasai na hakingepuuzwa.

Katika uchaguzi mkuu wa 1997 alishinda kiti cha Kajiado Kusini kwa kura 13,798 dhidi ya 10,232 za Sing’aru.

Ni muhimu kutaja kuwa kabla ya uchaguzi huo, Parpai alikuwa amehamia KANU kutoka DP, japo kwa muda mfupi akitarajia kumshinda Sing’aru katika mchujo wa chama.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2002, Parpai alijiunga na wimbi la National Rainbow Coalition (NARC) akiwa na Saitoti na wanachama wa chama cha Liberal Democratic Party (LDP) waliopinga uamuzi wa Rais Moi kumchagua limbukeni wa siasa Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake.

Narc iliposhinda Kanu, aliteuliwa waziri wa usimamizi wa wafanyakazi. Waziri msaidizi wake alikuwa Morris Dzoro, mbunge wa Kaloleni.

Lakini miezi michache baada ya kuapishwa, waziri huyo aliugua na kukimbizwa katika Nairobi Hospital alikogunduliwa kuwa na saratani.

Kifo chake Agosti 2003 kiliyumbisha nguvu za kisiasa za Kibaki katika eneo la Kajiado. Katika Baraza la Mawaziri la Kibaki, Parpai anabaki kuwa waziri ambaye uwezo wake kama waziri haukupimwa.

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Kingi atikisa siasa za Kilifi na Mombasa...

Saudia kuruhusu mahujaji milioni 1

T L