• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:15 PM
WALIOBOBEA: Poghisio alivyoleta mageuzi katika sekta ya ICT Kenya

WALIOBOBEA: Poghisio alivyoleta mageuzi katika sekta ya ICT Kenya

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

SAMUEL Losuron Poghisio alijiunga na Baraza la Mawaziri mnamo 2008, katika muhula wa pili wa Rais Mwai Kibaki.

Aliteuliwa kufuatia Muafaka wa Kitaifa ambao ulianzisha serikali ya muungano baada ya uchaguzi uliozua ghasia mwaka wa 2007, ambao Kibaki alikuwa ametangazwa mshindi.

Poghisio alipewa wizara ya Habari na Mawasiliano, jambo ambalo lilishangaza kwa kuwa wizara hiyo inachukuliwa kama uti wa shughuli za serikali na sekta ya kibinafsi nchini Kenya, ikidhibiti habari ambazo Wakenya wanaweza kupata katika jukwaa wanalochagua.

Haya yote sasa yalikuwa katika mikono ya mshirika wa muungano. Wizara hiyo ilihusika na shughuli muhimu kama vile Tume ya Mawasiliano ya Kenya sasa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya) ambayo inathibiti mawasiliano ya simu na utangazaji miongoni mwa majukumu mengine.

Kiongozi wa chama cha Poghisio, Kalonzo Musyoka, alikuwa makamu wa rais na ilikuwa wazi kuwa washirika wake wangepewa nyadhifa kubwa.

Poghisio alitwaa usukani wa wizara hiyo wakati mgumu katika historia ya Kenya.

Matukio kadhaa yalikuwa yakitendeka nchini na kote ulimwenguni. Si ajabu alipewa mawaziri wawili wasaidizi George Khaniri na Dhadho Godhana.

Katibu wa wizara hiyo alikuwa Bitange Ndemo, mtaalamu katika sekta ya ICT.

Ulikuwa wakati ambao taharuki kati ya serikali na wanahabari ilikuwa imetanda.

Serikali ilitaka kudhibiti shughuli za wanahabari, hasa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi zilizokuwa zimekumba nchi.

Kazi ya kwanza ya Poghisio ilikuwa kuhakikisha sheria ya kusimamia habari Kenya imepitishwa.

Nchi hii pia ilikuwa ikipatia changamoto za usalama kuhusiana na matumizi ya simu za mkono.

Watu walikuwa wakilengwa na wahalifu wa simu kutokana na ukosefu wa mchakato halisi wa usajili na njia ya pekee ya kukomesha hali hii ilikuwa kusajili rasmi wamiliki wote wa laini za simu.

Poghisio alishughulikia suala hilo, akisema usajili huo ungelinda umma kutokana na vitisho vya ugaidi, dawa za kulevya, ulanguzi wa pesa, jumbe za chuki na uhalifu mwingine uliohusishwa na simu za mkono.

Kufikia mwaka wake wa tatu katika wizara hiyo, Poghisio, ambaye alikuwa amehudumu kama waziri msaidizi wa Elimu ya Juu, Sayansi ya Tekinolojia kati ya 2,000 na 2,002, alikuwa katika harakati ya kufanya Kenya kuwa kituo cha ICT eneo la Afrika Mashariki kwa kuongeza upatikanaji na kasi ya intaneti.

Mwaka wa 2008, serikali iliidhiinisha kuanzishwa kwa jiji la Konza Technology City kama mradi muhimu wa Ruwaza ya Kenya ya 2030. Mwaka wa 2009, Rais Kibaki alianzisha ujenzi wa Konza Technopolis katika eneo la Malili, Machakos.
Bodi ya Mamlaka ya Konza Technopolis (KoTDA) iliundwa kufanikisha ujenzi wa jiji hilo.

Poghisio aliyezaliwa katika mwaka wa 1958, alisomea shule za msingi na upili Uganda kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere mwaka wa 1978 kusomea Sayansi ya Mimea na Wanyama.

Mwaka wa 1989 alijiunga na Wheaton College, Amerika kusomea digrii ya uzamili katika Mawasiliano kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Lincolin nchini humo kwa digrii nyingine ya uzamili katika Thiolojia.

Lakini alifanya kazi Kenya, kwanza kama mwalimu katika shule ya sekondari ya Chewoyet, Pokot Magharibi na kisha mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Daystar kabla ya kujiunga na siasa mwaka wa 1988 alipochaguliwa mbunge wa Kacheliba kwa tiketi ya chama cha Kanu lakini akapoteza kiti chake baada ya miezi minne alipofukuzwa chamani kwa kulaumiwa na serikali ya Rais Daniel arap Moi kwa kupendelea jamii yake ya Pokot katika ugavi wa chakula cha msaada.

Alichaguliwa seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi katika uchaguzi wa 2017 na akawa kiongozi wa Wengi katika seneti.

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Uteuzi wa Omar, Shahbal katika EALA...

PENZI LA KIJANJA: Ashiki ni kama pombe, ukilewa...

T L