• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
WALIOBOBEA: ‘Sirkal’ alipokataa wadhifa serikalini

WALIOBOBEA: ‘Sirkal’ alipokataa wadhifa serikalini

KWA HISANI YA KENYA YEARBOOK

NCHINI Kenya, nyadhifa za uwaziri haziwezi kuchukuliwa kama zinazotoshana- au kuwa sawa.

Kila moja ina ushawishi wake, na hii pengine inaelezea kwa nini baadhi ya nyadhifa za uwaziri huwa zinang’ang’aniwa. Wizara hizo ni kama fedha, usalama wa ndani, afya, kawi na elimu ambazo kwa kawaida husimamiwa na watu wa karibu na rais.

Hivyo basi, kupata moja ya nyadhifa hizi ni thibitisho la imani ya mtu serikalini. Rais huwa anasawazishwa kati ya utendaji na uaminifu. Ni kwa msingi huu ambapo uhusiano kati ya Joshua Orwa Ojode na Mwai Kibaki unaweza kutazamwa.

Kufikia wakati alikufa katika ajali ya ndege mnamo Juni 10 2012, Ojode( alikuwa na umri wa miaka 53) alikuwa waziri msaidizi aliyesimamia utawala wa mikoa na usalama wa ndani. Mkubwa wake, Waziri George Saitoti, alikuwa amehudumu kama makamu rais kwa miaka 13 kabla ya kuteuliwa katika wadhifa huo.

Kibaki alikuwa na imani kwamba wawili hao (Ojode na Saitoti) walitosha kusimamia wizara hiyo muhimu inayoshughulikia usalama katika kona zote za nchi. Baadhi ya idara zilizo chini ya wizara hiyo ni Huduma ya Taifa ya Polisi na Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS).

Ojode, aliyefahamika kwa jina maarufu Sirkal – msimbo wa jina Serikali, kutokana na uungaji mkono wake sugu wa Serikali ya Muungano iliyoongozwa na Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga – alikuwa mchapa kazi. Wakati mmoja aliambia bunge akijibu maswali aliyoulizwa kama waziri msaidizi, kwamba hajawahi kuwa na wakati wa kuharibu hata sekunde moja. Sirkal hakuwa na shughuli nyingi katika wizara aliyohudumu pekee; alikuwa akichangia sana bungeni.

Alikuwa akiwasilisha miswada na kuuliza maswali. Alijaribu kushawishi wabunge kuunda Kamati Teule ya kuchunguza kashfa ya Anglo Leasing ambayo Kenya ilipoteza mabilioni ya pesa katika uuzaji bandia. Hakuwa akiogopa mizozo.

Wakati mmoja Septemba 2002, miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu, gazeti maarufu la kila siku lilikuwa na kichwa, ‘ Kanu yaonywa kuhusu machafuko’.

Habari hiyo ilishangaza wachanganuzi wa kisiasa kwa sababu ilitoka kwa mwanachama mpya katika chama hicho tawala.

Onyo hilo lilitoka kwa mbunge wa Ndhiwa Joshua Orwa Ojode aliyekuwa ametabiri kuporomoka kwa chama kilichokuwa kimetawala tangu uhuru kufuatia hatua ya Rais Moi kuwaacha wanasiasa maarufu waliokuwa wakimezea mate urais akiwemo makamu rais aliyekuwa amehudumu kwa miaka mingi George Saitoti.

Kibaki alipovunja baraza la mawaziri mwaka wa 2005 baada ya kura ya maamuzi katiba mpya kushindwa, alimteua Orwa Ojode kuwa waziri wa Mazingira huku akimtema kigogo wa siasa wa eneo la Nyanza , Raila, ambaye kufikia wakati huo alikuwa Waziri wa Barabara, Ujenzi na Makao. Ojode alikataa uteuzi huo, kuwaunga wanachama wengine wa chama cha Liberal Democratic Party (LDP) ambao walikuwa wamefutwa.

Baadhi ya wachanganuzi wanasema kwamba Ojode angekubali wadhifa huo lakini alishawishiwa kuukataa na mibabe wa siasa katika jamii ya Waluo.

Baada yaserikali ya muungano kuundwa kufuatia ghasia za uchaguzi mkuu wa 2007, Ojode aliteuliwa waziri msaidizi wa wizara ya usalama wa ndani ambayo alihudumu hadi alipofariki katika ajali ya ndege Juni 10, 2012.

  • Tags

You can share this post!

Jumuiya ya kaunti za Pwani: Raia wanataka kuona vitendo,...

Ebola: ‘Lockdown’ yanukia Kampala

T L