KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK
ALIPOZALIWA mwana wa Ngina Muhoho na Mzee Jomo Kenyatta miaka ya mwisho ya ukoloni Oktoba 1961, ni Mwai Kibaki, ambaye wakati huo alikuwa Afisa Mkuu wa chama cha Kenya African National Union (Kanu), aliyependekeza apatiwe jina ‘Uhuru’.
Hii ilikuwa ni kuadhimisha uhuru uliokuwa ukinukia kwa watu wa Kenya. Lakini alipompa jina Uhuru mwaka wa 1961, Kibaki hakukisia kwamba miaka mingi baadaye, siasa zingemtenganisha na mtoto aliyepakata katika mikono yake, kabla ya kuwaleta karibu kwa njia nyingi, au kijana huyo angefuata nyayo zake kwa njia nyingi.
Uhuru Kenyatta alitumia miaka mingi ya utotoni akiwa na baba yake katika viwanja vya ndege na hafla za umma akisalimiana na Mawaziri, wakuu wa usalama na maafisa wakuu wa serikali, na kukutana na marais wa nchi tofauti na mabalozi, kijana Kenyatta alitazama kwa makini itifaki za siasa na serikali.
Baada ya baba yake kufariki mwaka wa 1978, Kenyatta alibaki katika kivuli bila kuonekana sana. Alionekana mara moja kwa mwaka katika Majengo ya Bunge kuadhimisha kifo cha baba yake kando ya Rais Daniel arap Moi na watu wa familia ya Kenyatta.
Alifanya kazi kwa muda mfupi kama karani wa benki baada ya kuhitimu chuo kikuu na kabla ya kuanzisha Wilham Kenya Limited, aliyotumia kununua na kuuza nje ya nchi mazao ya kilimo.
Alitokea, japo kwa muda mfupi, miaka 20 baadaye, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyogonga vichwa vya habari. Rais Moi, wakati huo alikuwa akikosolewa vikali kwa kukwamilia mamlakani kwa miaka mingi na kundi la wanasiasa walioongozwa na aliyekuwa makamu rais Jaramogi Oginga Odinga wakishinikiza nchi kurudia demokrasia ya vyama vingi.
Mifereji ya misaada ilikuwa imekauka na kulikuwa na taharuki ya kisiasa na hofu ya ujio wa hali isiyotabirika.
Ni katika hali hiyo ambapo taarifa ya habari iliyotiwa saini na Kenyatta na wana wa wanasiasa wa enzi za uhuru na mawaziri, Tom Mboya na Argwings Kodhek ilitokea.
Wakati umefika, walisema, wa utawala wa zamani kupisha damu mpya- Kanu na nchi kuwa na pumzi mpya.
Taarifa hiyo ilishtua nchi. Ilichukuliwa kuwa shambulio la moja kwa moja kwa Rais Moi, ambalo lilikuwa la kijasiri sana ikizingatiwa kwamba Moi alikuwa akiogopwa sana, uhusiano wake wa karibu na kihistoria kati ya familia za Moi na Kenyatta na kwa ukatili wa serikali ya Kanu wakati huo.
Chama cha Kanu kilikasirika, na msemaji wake alikemea vijana hao akisema kwamba walizaliwa katika utajiri na kwa hivyo hawakufahamu ukweli wa mambo.
Katika mashambulizi yaliyofuatia, Kenyatta alirudi nyuma na kunyamaza.
Hata hivyo, Wakenya walikuwa wameona dalili, na swali lilibaki kuwa ni lini na sio iwapo alipanga kugombea kiti cha kisiasa.
Kilichoshtua zaidi ni wakati familia yenye nguvu ya Kenyatta ilitoa taarifa kueleza kuwa wangemuunga aliyekuwa Makamu Rais na Waziri wa Fedha Mwai Kibaki, ambaye alikuwa amejiuzulu kama Waziri wa Afya mnamo Desemba 1991 kuunda chama cha Democratic Party (DP), kumpinga Moi kwenye uchaguzi wa vyama vingi vya kisiasa wa 1992.
Ilionekana kuwa uhusiano wa familia za Moi na Kenyatta ulikuwa umeharibika kiwango cha kutorekebika.
Hata hivyo, Kenyatta hakugombea kiti cha Ubunge cha Gatundu ilivyotarajiwa. Moi alishinda upinzani uliokuwa umegawanyika; kwa mara nyingine, Kenyatta alienda chini ya maji lakini kulikuwa na dalili kwamba uhusiano ulikuwa umerejea Kenyatta alipoibuka mwaka wa 1997 kugombea kiti cha Gatundu Kusini kwa tiketi ya Kanu badala ya DP cha Kibaki wengi walivyotarajia. (Itaendelea Jumapili ijayo)
Subscribe our newsletter to stay updated