• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
WALLAH BIN WALLAH: Ukitaka kuzifanya kazi zako ziwe bora zaidi, basi lazima ujiboreshe mara kwa mara!

WALLAH BIN WALLAH: Ukitaka kuzifanya kazi zako ziwe bora zaidi, basi lazima ujiboreshe mara kwa mara!

NA WALLAH BIN WALLAH

KINOLEWACHO hupata.

Na kikipata hukata! Hivyo ndivyo wasemavyo wataalamu wanaoamini na kuthamini kwamba ukitaka zana zako za utendakazi zikufae, lazima ziwe katika hali njema.

Ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Ubora wa chombo chochote ndio husababisha ubora wa utendakazi. Hali ni vivyo hivyo kwa mwanadamu pia. Mtu yeyote anayefanya kazi kwa makini kitaalamu ndiye ambaye kazi yake huwa bora zaidi maishani!

Mtu ambaye hafanyi kazi yake kwa ufundi na umahiri, kazi yake haiwezi kuzalisha natija na ufanisi wowote!

Ili kazi iwe bora ya kuvutia lazima ifanywe kwa ujuzi, akili na kitaalamu kutoka kwa mtaalamu. Mpanda ovyo huvuna ovyo! Naye mpika ovyo huivisha ovyo!

Kazi hizi tunazozifanya maishani mwetu zinaweza kuwa bora zenye faida kubwa zaidi endapo sisi watendakazi tungetumia ubora na ujuzi wa kiwango cha juu sana.

Aghalabu kazi zetu huharibika na kukosa ubora kwa sababu sisi wenyewe hatujiongezei ubora wa kujinoa kila mara! Tusiridhike na hali tuliyo nayo tu. Ujuzi na utaalamu ni vitu vinavyopaliliwa kila wakati!

Ni kama kisu ambacho ukikitumia tu bila ya kukinoa, kitakuwa butu wala hakitakata tena!Maathalani, mwalimu anayewafunza tu wanafunzi bila ya yeye mwenyewe kuendelea kujifunza ataalamike zaidi, hawezi kuwa mwalimu bora! Naye mwanafunzi asiyejibidiisha kujifunza kila mara hawezi kuwa bora wa kufuzu mtihani vizuri!Ni muhimu kila mtu anayetaka kufanya kazi zake ziwe bora zaidi, yeye pia ajiboreshe kila mara!!!!

  • Tags

You can share this post!

Serikali kuuza taasisi bila kuhusisha Bunge

Seneta Omtatah kuelekea kortini kupinga mpango wa...

T L