• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
Wanakuza Hass Avocado kuwafaa wakazi wa Gusii

Wanakuza Hass Avocado kuwafaa wakazi wa Gusii

NA WYCLIFFE NYABERI

IKIWA umewahi kusafiri majira ya jioni kutoka Kisii kwenda Nairobi siku yoyote ile, huenda macho yako yalitua kwenye magunia makubwa meupe ambayo yameegeshwa katika maeneo teule kando kando mwa barabara.

Ndani ya magunia haya, huwa pamejazwa maparachichi ambayo kwa kawaida itahitaji angalau wanaume wanne waliokula wakashiba ndiposa wanyanyue moja kulipakia kwenye lori.

Maparachichi haya ni yale ya kawaida ambayo thamani yake sokoni si kubwa ikilinganishwa na yale ya hass, ambayo yamepata umaarufu mkubwa hasa kwa wakulima wanaofanya kilimo biashara.

Baada ya kushuhudia mafadhaiko wanayopitia wakulima wa maparachichi ya kawaida, kundi moja la wafanyabiashara katika mji wa Keroka, wengi wao wazawa wa Mlima Kenya na maeneo ya Ukambani, waliona heri kuanzisha mradi wa kuwakuzia wakulima wa Gusii miche ya maparachichi ya hass ili kufanikisha kilimo biashara katika eneo hilo.

Safu ya Akilimali ilizuru kikundi hicho cha Wema Imani Enterprises (WIE) katika nasari yao Bogeche, eneobunge la Nyaribari Masaba kupambanulia wasomaji wetu jinsi wanalenga kuinua jamii kwa kuhakikisha kuwa aina nzuri ya maparachichi ndiyo yanayokuzwa.

“Kikundi chetu ni cha watu 15. Wengi wetu hutoka Mlima Kenya ambapo kilimo cha maparachicghi ya hass kimenoga. Tumeona jinsi wakazi wa huko wametajirika kutokana na avocado hizi ilhali huku Kisii, wakulima wengi bado wanang’ang’ana na zile za kienyeji zisizo na manufaa tele,” Eliud Gitonga, meneja msimamizi wa mradi huo wa WIE anasema.

Walianza mradi huo miaka miwili iliyopita. Mmoja wa wanachama wao ambaye ni mzawa wa Kisii, alijitolea na kuwapa sehemu ya shamba lake kufanyia uzalishaji wa miparachichi yenye ubora unaohitajika.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Stephen Thiong’o anaeleza kuwa wao hujizalishia miparachichi ya hass kwa kutumia mbegu za maparachichi ya kiasili ambazo anasema ni mufti katika kuzindua awamu ya kuishia kuwa na miche bora ya Hass.

Wao huletewa mbegu hizi na vijana wa mtaani wanaoziokota masokoni na maeneo mengine zinakopatikana. Wanawalipa vijana mtaji fulani kwa kazi yao.

Mbegu hizi wanazipanda katika mifuko ya plastiki yenye udongo mzuri wenye rotuba. Baada ya miezi angaa mitatu kulingana mwenyekiti, miparachichi hiyo asili itakuwa imetimiza urefu wa futi mbili hivi.

Hatua inayofuata ni kusaka mparachichi wa hass ulio na ubora wa juu na kuvuna matawi wanayotumia kuzalisha ile asili.

 

Wanachama wa Wema Imani enterprises wakagua miparachichi yao ya hass katika nasari yao iliyoko Bogeche. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Matawi hayo kwa kizungu huitwa scions na kwa kuwa wanahitaji yaliyo na ubora mzuri, wao husafi risha scions zao kutoka Mlima Kenya.

Wakishafika shambani, wanaangalia kwa makini saizi zinazoweza kuingiana na ile mimea yao ya kienyeji.

Wakishachagua scions au badi hizo, wanahitaji nyembe na makaratasi ya plastiki.

“Sisi hukata mimea ile ya kienyeji katika kiwango cha urefu wa futi moja na nusu na kisha shina lake kuanzia juu katikati ukielekeza chini ili kuunda nafasi ya kupenyeza badi zile za hass.

Tunachonga badi hizo vizuri ili ziingie katika nafasi iliyoundwa katika mmea wa kienyeji.

Awamu ya tatu ni kufunga badi kwa karatasi za plastiki ili kuziunganisha na mmea asili ndiposa ishikamane.

Baada ya kipindi cha wiki tatu hadi tano, badi hizo ikiwa zilifungwa vizuri zitaanza kuchipuza majani, ishara kwamba zimeanza kunawiri na hapo miparachichi ya hass itapatikana.

Tangu kuanza kwa mradi wao, wameuza miparachichi 1,000 ya hass kwa Sh200 kila mmoja.

Hii iliwachumia kima cha Sh200, 000 pesa taslimu.. Walipoanza mradi wao, waliwekeza Sh70,000 tu. Kwa sasa wana zaidi ya miparachichi 3000 ya hass ambayo iko tayari shambani.

Mingi ya miparachichi yao wanawauzia watu wa karibu hapo na Bi Joyce Orucho ni mmoja wao.

“Niliasi ukulima wa majanichai na sasa miparachichi ndiyo tija yangu, miche yangu iko tayari kuzaa. Kwa muda mrefu nimekuwa nikichumia juani lakini hivi karibuni nitakula kivulini,” anasema Bi Orucho.

Kulingana na Bw Gitonga, lengo lao ni kuona kwamba wakulima wote wa parachichi Kisii wanakuza aina ya hass ili kuimarisha viwango vya mapato na hatimaye viwango vya maisha katika jamii.

  • Tags

You can share this post!

TANZIA: Mbunge afariki baada ya kugongwa na pikipiki

Ni wakati wa Harambee Starlets kung’aa – Beki

T L