• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:13 PM
WANDERI KAMAU: Tubuni makavazi ya uanahabari kukuza historia, mila zetu

WANDERI KAMAU: Tubuni makavazi ya uanahabari kukuza historia, mila zetu

Na WANDERI KAMAU

SEKTA ya uanahabari nchini ni miongoni mwa nguzo kuu ambazo zimechangia pakubwa katika uhifadhi wa historia ya Kenya.

Pasingekuwepo na sekta hiyo, pengine kumbukumbu kuhusu matukio muhimu nchini hazingekuwepo.

Tangu uhuru mnamo 1963, vyombo vya habari kama redio na magazeti vimenakili kila hatua ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo Kenya imepitia hadi ilipofikia iliko sasa.

Kwa mfano, Shirika la Utangazaji la KBC lina kumbukumbu pevu kuhusu matukio ya kisiasa yaliyofanyika nchini katika miaka ya sitini, sabini, themanini hadi sasa.

Vivyo hivyo, magazeti muhimu kama ‘Taifa Leo’, ‘Daily Nation’, ‘The Standard’, ‘People Daily,’ kati ya mengine yamechangia sana kwenye harakati za kuleta ukombozi wa kisiasa nchini.

Kutokana na mchango huo muhimu, kuna haja kubwa kwa serikali kubuni makavazi maalum kuhusu mchango uliotolewa na vyombo vya habari nchini.

Ni kutokana na mchango wa vyombo vya habari ambapo wale wanaorejelea kumbukumbu kuhusu matukio muhimu huwa wanapata mwanga na upevu wa yale yaliyojiri nyakati za hapo nyuma.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa licha ya uwepo wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), serikali imekuwa ikitilia maanani uwekezaji katika masuala ya kiteknolojia na kusahau juhudi za kuhifadhi historia na tamaduni zetu.

Kutokana na pengo hilo, imewalazimu wanahabari na watu waliobobea katika nyanja mbalimbali katika nyakati za hapo nyumba kufanya juhudi kuandika vitabu kwa gharama zao wenyewe.

Mfano mzuri ni mtangazaji mkongwe Leonard Mambo Mbotela, ambaye yuko kwenye harakati za mwisho mwisho kumalizia kuandika tawasifu yake iitwayo ‘Je, Huu ni Ungwana?’

Kwa yeyote ambaye amapata nafasi ya kumsikiliza Mzee Mambo akielezea safari yake katika utangazaji tangu miaka ya sitini, simulizi zake huwa zenye mnato sana. Huwa anazisimulia kama matukio yaliyofanyika jana.

Mojawapo ya simulizi hizo ni kuhusu jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya marehemu Daniel Moi mnao Agosti 1, 1982.

Ingawa kuna mamia ya vitabu ambavyo vimeandikwa kurejelea tukio hilo, hakuna kilichoeleza kwa kina kama anavyorejelea Mzee Mambo, kwani ni jambo ambalo yeye binafsi alilishuhudia.

Ili kuhifadhi na kuendeleza kumbukumbu kama hizo, kuna haja kubwa kwa serikali na wadau husika kubuni makavazi maalum yatakayoelezea mchango wa vyombo vya habari nchini.

Hiyo itakuwa mojawapo ya njia ya kuhifadhi na kuendeleza historia, turathi na utamaduni wetu.

[email protected]

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Wakenya watumie akili kabla ya mambo...

Zuma alazwa hospitalini baada ya kuugua gerezani