Na MARY WANGARI
IDADI ya watu wanaoandaa hafla za uchangishaji pesa za kugharamia matibabu imeongezeka pakubwa katika siku za hivi majuzi, huku mzigo wa gharama ya afya ukizidi kuwalemea Wakenya.
Iwe ni katika sehemu za ibada, kazini, makazi, mitandao ya kijamii na kwingineko, imekuwa kama ada kila uchao kupata matangazo ya kuomba msaada kuchangisha mamilioni ya fedha kugharamia malipo ya hospitali.
Uhalisia uliopo unajitokeza bayana hasa katika kizazi hiki cha utandawazi ambao umeufanya ulimwengu kuwa kijiji.
Si ajabu siku hizi mtu kujipata katika kundi zaidi ya moja katika mitandao ya kijamii anapotakiwa kusaidia kuchangisha mradi tu kusaidia familia, jamaa au marafiki waliolemewa baada ya wapendwa wao kulazwa hospitalini.
Kwa muda mrefu, mzigo wa kugharimia matibabu nchini umekuwa kero ambayo imewafilisisha raia wengi.
Familia nyingi zimelazimika kuuza mali yao yote na kutumia kila walicho nacho katika juhudi za kugharamia matibabu ya wapendwa wao hasa wanaougua maradhi sugu.
Hali pia imevurugika zaidi kutokana na janga la Covid-19 ambalo limesababisha madhara yasioelezeka kijamii na kiuchumi.
Katika baadhi ya visa vya kuvunja moyo, familia zimegubikwa na majonzi maradufu baada ya kupatwa na msiba, kisha usimamizi wa hospitali walimolazwa hasa katika hospitali za kibinafsi, kukatalia miili ya wapendwa wao.
Ndiposa umuhimu wa kuwepo mikakati kabambe ya kuwapunguzia Wakenya gharama ya matibabu hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.
Japo hospitali za kibinafsi huwa ghali, Wakenya hujipata hawana hiari ili kwenda huko kutafuta huduma bora za matibabu ikilinganishwa na hospitali za umma, katika juhudi za kuokoa wapendwa wao.
Serikali imepiga hatua katika juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini kuambatana na malengo ya Afya kwa Wote (UHC).
Mfano mzuri ni kupitia mswada mpya wa NHIF unaoagiza kila mwananchi mwenye umri kuanzia miaka 18 kujisajilisha na Hazina ya Afya Nchini.
Ingawa mswada huo una vipengele kadhaa vinavyohitaji kupigwa msasa ili kuwafaidi Wakenya kikamilifu, bila shaka ni ishara njema.
Isitoshe, wiki chache zilizopita, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa ilani kwa hospitali za kibinafsi zinazotoza ada ghali kupindukia na kukatalia miili ya wagonjwa wanapoaga kabla ya kukamilisha malipo.
Ili kutoa afueni kwa Wakenya, Bunge linapaswa kubuni sheria zitakazoweka ada mahsusi inayostahili kuzingatiwa na hospitali za kibinafsi kuhusu utowaji huduma mbalimbali.
Serikali pia inafaa kutumia vyema ushuru unaokusanywa kutoka kwa wananchi kuimarisha huduma za afya katika vituo vya umma.
Hii ni kupitia ukarabati wa miundomsingi, kuboresha utowaji huduma za afya, kuhakikisha kuwepo kwa dawa za kutosha na vifaa vya kisasa vya matibabu.