• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
WANTO WARUI: Serikali iwape vijana mazingira bora kuundia bidhaa nchini

WANTO WARUI: Serikali iwape vijana mazingira bora kuundia bidhaa nchini

NA WANTO WARUI

Kenya inajivunia vyuo vikuu vingi vya elimu vikiwemo vile vya umma na vya kibinafsi. Maelfu ya wanafunzi na wasomi wanapata shahada mbalimbali za masomo kutoka katika vyuo hivi vilivyo nchini na vingine katika nchi ambazo ni majirani wetu.

Hata hivyo, licha ya kufunzwa katika vyuo hivi na kupata maarifa ya kujiundia vitu, asilimia kubwa sana ya wale wanaofuzu bado iko barabarani ikitafuta kazi za kuajiriwa.

Ni jambo linaloshangaza kuona wananchi wenye shahada wakitaabika kutafuta kazi ilhali nchi ina rasilimali za kutosha.

Masomo yanayotolewa katika vyuo vikuu yanafaa kumwezesha mwanafunzi kuwa mbunifu wa ajira anapofuzu bali si kuwa mtegemezi.

Kuna shida kadhaa nchini ambazo zinatatiza ubunifu na utoaji wa ajira nchini. Mojawapo ya shida hizi ni ushuru wa juu sana. Serikali inatoza ushuru wa juu bidhaa nyingi humu nchini jambo ambalo linatatiza uundaji bidhaa.

Kwa mfano, unga wa mahindi unauzwa kwa bei ya juu sana nchini licha ya kuwa mahindi yanalimwa kwa wingi.

Kutokana na gharama ghali ya ukulima, usagaji, upakiaji na usafirishaji, pakiti moja ya unga ambayo haistahili kuuzwa zaidi ya sh70, sasa inauzwa maradufu.

Vilevile kuna bidhaa kadha wa kadha ambazo Wakenya wana uwezo mkubwa wa kutengeneza lakini inashindikana kutokana na sababu kwamba bidhaa hizo zikikamilika zitakuwa zimetozwa ushuru wa juu sana hata kuliko zile zinazotoka nje ya nchi.

Aidha, kuna baadhi ya wafanyabiashara laghai na matapeli ambao wanapitia njia za mkato kuingiza bidhaa nchini na hivyo basi kuziuza kwa bei ya chini sana. Bidhaa kama vile nguo na vifaa vya kielektroniki zinaweza kupatia wataalamu wetu ajira na hata vijana wengi nchini.

Kutokana na sababu kwamba bidhaa hizi ni ghali mno kuzitengenezea nchini, ama ufisadi unachangia kuingiza bidhaa nchini, elimu yetu inaishia kuwa ya bure tu au ya utumwa.

Vyuo vyetu vikuu vinaachiwa tu majina makubwa yasiyo na maana kwani wanaofuzu katika vyuo hivyo wanaishia tu kuwa watumwa wa watu wengine.

Haja kubwa ya elimu hasa elimu inayotolewa katika vyuo vikuu ni kusuluhisha shida na kutatua matatizo yanayoitinga jamii.

Ikiwa elimu hiyo haiwezi kufanya hivyo ama inamfanya mtu kuwa mtumwa wa watu wengine basi elimu hiyo itakuwa haina maana.

Wanazuoni wa taifa hili wanakiri kuwa Kenya ina uwezo mkubwa wa kujiundia bidhaa zake na kupunguza utegemezi wa kibiashara kutoka kwa mataifa mengine.

Tuelekeapo uchaguzini mwakani, serikali mpya inafaa kuunda sera madhubuti ambazo zitawawezesha wataalamu wetu kuunda bidhaa nchini kwa kudhibiti ushuru na ufisadi.

You can share this post!

Tetemeko kubwa lapiga Haiti na kuua watu 1,200

TAHARIRI: Wanaotoa chanjo watoe habari zote