• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Yesu Wa Tongaren sasa ni huru kusafisha dhambi za Wakenya

Yesu Wa Tongaren sasa ni huru kusafisha dhambi za Wakenya

NA SAMMY WAWERU

MHUBIRI Eliud Simiyu maarufu kama Yesu Wa Tongaren ameachiliwa huru baada ya Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kusema haina ushahidi kumfungulia mashtaka.

Hakimu Mkuu mahakama ya Bungoma, Tom Olando Jumanne, Mei 16, 2023 aliagiza mchungaji huyo kuachiliwa huru kutoka seli ya polisi.

Hakimu Olando alitoa amri hiyo baada ya DPP kusema ushahidi uliowasilishwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) hauna msingi wowote kumfungulia mashtaka Yesu Wa Tongaren.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, pia iliamuru faili ya kesi hiyo kufungwa.

Aliwakilishwa na aliyekuwa mgombea wa urais 2022 kwa tikiti ya Roots Party Kenya, Wakili Prof. George Wajackoyah.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuachiliwa huru, Yesu Wa Tongaren alieleza kutoridhishwa kwake na hatua ya kukamatwa licha ya kushirikiana kwa karibu na maafisa wa polisi.

Katika kauli iliyozua ucheshi, alifichua kwamba Jumamosi, Mei 13, 2023 aliandamana na askari nyumbani kwake ili uchunguzi kufanywa na walichopata ni sadaka ya Sh225.

“Mbali na sadaka ya Sh225, pia walipata nyanya na vitunguu,” Yesu Wa Tongaren alielezea.

Jumamosi, ni siku yake ya Sabato.

Mei 12, alipofikishwa kortini ofisi ya DPP ilihoji pasta huyo mcheshi anachunguzwa kwa madai ya kupotosha waumini wake.

Hali kadhalika, polisi walidai anaandamwa na tuhuma za biashara haramu ya pesa na kupokea fedha za uhalifu.

Alikamatwa Mei 10, 2023 na amekuwa seli tangu wakati huo.

Kamanda wa Polisi wa Bungoma Francis Kooli Mei 8, 2023, alimtaka mchungaji huyo kujiwasilisha katika kituo cha polisi cha Bungoma “baada ya malalamishi kuibuliwa kwamba anatoa mafunzo ya itikadi kali”.

Kukamatwa kwake kulijiri wakati ambapo eneo la Pwani, msitu wa Shakahola, Kilifi ufukuzi wa maiti unaendelea.

Mhubiri tata Paul Mackenzie anahusishwa na maafa ya washirika wake, kupitia hadaa za dini potovu.

  • Tags

You can share this post!

Vidokezo mahususi kwa vijana kupunguza uzani

Polisi wachunguza kifo cha raia usalama ukidorora

T L