• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:50 AM
ZARAA: Aliachana na mahindi kahawa iliponyanyuka

ZARAA: Aliachana na mahindi kahawa iliponyanyuka

NA PETER CHANGTOEK

KAUNTI ya Narok hujulikana kwa uzalishaji wa ngano, mahindi na viazi.

Hata hivyo, kuna wakulima walioacha ukuzaji wa mahindi na kujitosa katika ukuzaji wa kahawa. Joseph Soi ni mmoja wao.

Mkulima huyo amekuwa akikuza kahawa kwa zaidi ya miaka mitano, katika eneo la Olemekenyu, eneobunge la Narok Kusini, Kaunti ya Narok.

Yeye ni makamu mwenyekiti wa Baraka Narok South Coffee Cooperative Society. Kundi hilo lina wanachama zaidi ya 120, ambao walijitosa katika ukuzaji wa mmea huo.

“Tulianzisha ushirika huu mwaka 2014, na tukaendelea hadi sasa. Tulitengeneza kitalu cha miche 2014 na tukaanza kuipanda miche 2015. Nilianza kwa shamba nusu ekari, kisha ekari moja, na kwa sasa, nina ekari tatu,” asema Soi, 52.

Anasema kuwa, huchuma kahawa katika shamba ekari mbili, na mikahawa aliyoipanda miezi michache iliyopita, itaanza kuzaa matunda ya kahawa kuanzia Mei.

“Humaliza mwaka mmoja na nusu tangu ipandwe ili ianze kuchumwa. Baada ya miaka miwili ndipo huanza kuzaa kahawa kwa wingi,” asema, akiongeza kuwa, mkahawa unapozidi kukua, ndipo mazao yanapozidi kongezeka.

Soi anasema kuwa, kwa wakati huu, huchuma kahawa kilo 5 hadi 7 kutoka kwa mkahawa mmoja kwa msimu mmoja.

“Huchuma kila baada ya wiki mbili kuanzia kilo 1,400 hadi kilo 1,600. Huanza kuchanua maua mwezi wa pili, na huchumwa mwezi wa nane,” afichua mkulima huyo.

Anaongeza kuwa, yeye huchuma kahawa kwa muda wa miezi minne mfululizo.

“Kuanzia mwezi wa nane hadi Desemba huwa na pesa,” adokeza.

Mkulima huyo hutumia mbolea asilia – samadi ya ng’ombe wakati anapoipanda miche ya mikahawa. Anongeza kuwa, baada ya kuipanda, huhakikisha kuwa anapalilia ili kuyaondoa magugu shambani. Baada ya miezi sita, hutumia mbolea aina ya CAN kwa mikahawa yake.

“Hutumia gramu 50 za CAN, na baada ya mimea kukua na kuanza kuzaa kahawa, huweka gramu 100 za CAN,” asema Soi, ambaye hukuza aina ya Batian.

Anaeleza kuwa, mikahawa ikitunzwa vyema, huenda isiathiriwe na magonjwa.

“Tulifunzwa juzi kuwa tunafaa kutunza kwa kunyunyizia dawa mbalimbali kwa muda wa miezi sita. Kuna za wadudu, za magonjwa na za kufanya kahawa kuwa kubwa,” asema.

Baada ya wakulima hao kuzichuma kahawa zao, hukusanywa na maafisa wa chama hicho cha ushirika, na kupimwa baada ya kila miezi miwili, na kupelekwa kwa kampuni inayozinunua.

Soi anasema kuwa, huyauza mazao yao kwa kampuni ya CMS – Coffee Millers Society, iliyoko mjini Eldoret.
Anafichua kuwa, kuna wakati ambapo walilipwa Sh490 kwa kilo moja ya kahawa.

Hata hivyo, kuna wakati ambapo huuza kwa Sh450, Sh430 hadi Sh270 kwa kilo, kuambatana na msimu.

Anasema kuwa, kuna changamoto kadhaa katika zaraa hiyo. Bei za juu za pembejeo za kilimo, kama vile mbolea, dawa, n.k, ni miongoni mwa changaamoto anazosema wanapitia.

Aidha, hawajapata mashine bora za kuchakata. Hata hivyo, anasema aliinunua mashine ya kuondoa maganda ya kahawa kwa Sh40,000. Mashine yenyewe inaweza kuondoa maganda ya kahawa takribani kilo 1,000 kwa siku.

Anaomba serikali ya Narok kuwapa usaidizi wakulima wa kahawa.

“Kuna mashine inayouzwa na Sh1 milioni; tukipata mashine hiyo tutakuwa tumesaidika sana. Tungepewa mbolea pia,” asema Soi.

Wao hushurutika kununua mbolea na dawa za kunyunyizia kahawa kutoka Kericho kwa sababu Kaunti ya Narok haijakumbatia uzalishaji wa kahawa, na hivyo ni nadra kuzipata katika kaunti hiyo.

Kwa wakati mwingine, wakulima hao huchukua mbolea kutoka kwa kampuni ili fedha za mbolea na dawa hizo ziondolewe kutoka kwa fedha wanazolipwa.

“Nina wanachama 120 lakini wanaouza kahawa tayari ni wanachama 75, lakini hivi karibuni, nitakuwa na zaidi ya wanachama 200. Mwenyekiti wetu ni Philip Maritim, mwekahazina ni Gideon Ng’etich, na katibu ni Simon Ng’etich,” aeleza.

Anapania kuongeza kiasi cha shamba na kuwa na ekari tano hadi kumi za mikahawa.

“Sina shida kulipa karo za shule. Siku hizi mimi sikuzi mihindi. Kahawa hazilinganishwi na mahindi; nikiuza kahawa gunia moja, hununua chakula kinacholiwa mwaka mmoja. Gunia moja huuzwa kwa takribani Sh40,000 – hizo ni pesa nyingi. Tumewahamasisha wakulima kukuza kahawa. Hununua miche kutoka kaunti ya Nandi kwa Sh35 kwa kila mche,” afichua mkulima huyo.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Wachina huwania nyama ya sungura wao kila wakati

MITAMBO: Mtambo safi katika uundaji lishe toka makapi ya...

T L