• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
ZARAA: Atambua vinyonga ni dawa ya wadudu shambani

ZARAA: Atambua vinyonga ni dawa ya wadudu shambani

NA SAMMY WAWERU

SHAMBA la Charles Mburu ni bustani ya mseto wa matunda, mengi akiwa anayakuza kwa minajili ya biashara.

Limesheheni matunda kama avokado, ndizi, machungwa, mapapai, mapera, matundadamu, matikiti ya pepino, karakara, stroberi, matufaha, zabibu, maembe, komamanga na ndimu.Mburu anasema ana zaidi ya aina 20 ya matunda, katika shamba lake lililoko Ndeiya, Kaunti ya Kiambu.

“Nilirithi kilimo cha matunda kutoka kwa babangu, aliyepokezwa na babu,” adokeza.

Kijiji cha Kamugumo, anaendeleza ukuzaji wa matunda kwenye ekari mbili na nusu.

Safari katika kilimo iling’oa nanga 2008 baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne (KCSE), ambapo aliendeleza nyayo za baba yake na babu.Kupanua kiwambo kunasa mapato zaidi, alijumuisha ufugaji wa sungura.

“Mwaka wa 2013, nilishiriki zoezi la uchaguzi kama karani na mshahara niliopokea nilitumia kuanzisha mradi wa sungura,” aelezea.

Anafichua kwamba ilimgharimu mtaji wa Sh48, 000 kuanza kufuga sungura wapatao 200. Hata hivyo, Mburu anasema ni mojawapo ya ufugaji ambao mkulima asipokuwa makini katika masuala ya soko ataishia kusaga meno.

“Walipokomaa, nilifanikiwa kuuza sungura 20 pekee. Waliosalia tuliwala na wengine kuwapa mbwa,” akumbuka hasara aliyokadiria.Mburu vilevile alikuwa amejaribu bahati yake katika ufugaji wa kuku wa nyama (broilers), japo biashara hiyo pia ilimpiga chenga.Ukuzaji wa matunda ndio ulimtuliza.

Huku gharama ya kilimo ikiendelea kuwa ghali kufuatia kupanda kwa bei ya pembejeo, Mburu ametambua mbinu maalum kukabiliana na kero ya wadudu.Matumizi ya vinyonga (chameleons), ni mfumo asilia wenye mvuto aliovumbua na anakiri unamletea afueni.Wengi wakichukulia wanyama hao kuwa adui, kwake ni dhahabu.

“Nina zaidi ya vinyonga 100 kwenye shamba langu,” afichua.

Anasema wanyama hao wana manufaa makubwa hasa mitunda inapochana maua.Ni kipindi ambacho wadudu hukita kambi, wakisaka chakula.

Mlo wa kinyonga ni wadudu, na Mburu anawatumia kukabili wadudu aina ya lacewing wa kijani na hudhurungi.

Huwakusanya anapokutana nao, na anafichua kwamba ana leseni ya Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS). Wadudu sugu kwa matunda ni vithiripi, nzi weupe, vidukari, vidung’ata, kati ya wengine.

Akisifia mfumo huo asilia, Damaris Kagendo mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro) tawi la Katumani, hata hivyo anasema unafanya bora endapo idadi ya vinyonga ni ya juu kuliko wadudu.

“Kimsingi. chakula cha kinyonga ni wadudu na kuwa nao shambani ni mojapo ya mbinu kuwadhibiti,” mdau huyo asema.

Wakati wa mahojiano na Akilimali, Mburu alikiri kwamba wanyama hao wamekuwa wa manufaa makubwa kufanikisha kilimo chake cha matunda.

“Ufanisi wa mavuno zaidi ya asilimia 65 bila kutumia kemikali, ina maana kuwa matumizi ya kinyonga ni faafu,” Mburu asisitiza.

Kando na msimu wa miti kuchana maua, mkulima huyo pia hutilia maana inapotunda.

Aidha, huwahifadhi kwa kukuza nyasi za mabingobingo (Napier), msimu wa mavuno unapoisha.Mbinu zingine anazotumia kukabiliana na wadudu ni kuunda dawa asilia kwa kutumia majani, jivu, makaa ya miti maalum, na kinyesi cha nguruwe.

“Pilipili hoho (zile kali) na mmea aina ya Mexican Marigold, ni adui wa wadudu.”

Hukuza vitunguu kwenye ncha ya shamba na kati ya mimea, harufu ya kiungo hicho cha mapishi ikitajwa kuchangia kufurusha wadudu.Kufuatia bunifu za mkulima huyo mwenye Stashahada ya Masuala ya Uhandisi kuzalisha matunda kiasilia, East African Growers Ltd ndio wanunuzi wake wa mazao.

  • Tags

You can share this post!

Muungano maarufu KEWOPA wazindua kampeni ya kuvumisha...

Wabunge wafuatilia matumizi ya Sh 55B siku za mwisho za...

T L