• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
ZARAA: Kazi ilikosekana, akajipa ya ukulima na wala hajuti

ZARAA: Kazi ilikosekana, akajipa ya ukulima na wala hajuti

NA PETER CHANGTOEK

BAADA ya kusaka ajira kwa muda mrefu pasi na mafanikio, Jackson Sawe aliamua kujitosa katika ukuzaji wa mikarakara.

“Nilisomea taaluma ya Teknolojia ya Mawasiliano na ualimu, lakini nilikufa moyo kwa kutafuta ajira, na kuamua kujihusisha na uzalishaji na kuisadia jamii yangu. Nilichagua mikarakara, shughuli niliyoanzisha 2017 katika shamba robo ekari,” aeleza Sawe.

Anaongeza kuwa, amefanikiwa kuwahamasisha vijana 13 kujitosa katika zaraa hiyo, na kwa sasa, wanajishughulisha na shughuli hiyo chini ya mwavuli unaojulikana kwa jina Organic Passion Fruits Bomet Ltd, katika Kaunti ya Bomet.

Anasema kuwa, shamba ekari moja linaweza kutumika kuikuza mimea 800 ya mikarakara. Kwa hivyo, shamba lake robo ekari aliloanza nalo, lilichukua miche 200, aliyoinunua kwa Sh50 kila mmoja.

Mtaji alioutumia kuanzisha shughuli hiyo ulikuwa Sh30,000 uliojumuisha fedha alizotumia kununua vikingi, mbolea na dawa mbalimbali.Mkulima huyo anadokeza kuwa, aliamua kuikuza mikarakara aina ya Giant Ester, anayosema huzaa matunda kuanzia kilo mbili hadi tatu.

Jackson Sawe akiwa katika shamba lake katika eneo la Kipyosit, Kaunti ya Bomet. PICHA | PETER CHANGTOEK

Sawe anasema aina hiyo ya mikarakara huzaa matunda kila wakati.

“Sijawahi kukosa kuchuma kuanzia Aprili 2021. Hailinganishwi na ile inayoatikwa ambayo huweza kukauka baada ya mwaka mmoja baada ya kuchumwa,” asema, akiongeza kuwa, mikarakara aina ya Giant Ester, aghalabu haiathiriwi na magonjwa wala kuvamiwa na wadudu kwa urahisi.

Anaongeza kuwa, aina hiyo huwa na ganda gumu linalozuia wadudu kuyadunga matunda hayo kwa urahisi.

“Matunda ya Giant Ester ni makubwa na matunda machache huhitajika kujaza uzani wa kilo moja na pia hufikia asilimia 90 ya kiwango kinachotakikana ili kuuzwa nje,” asema, akiongeza kwamba, kilo moja huuzwa kwa Sh100-Sh120.

Sawe, anayeendeleza zaraa hiyo katika eneo la Kipyosit, anasema kuwa, ili kupata mazao bora, hutumia mbolea asilia kila baada ya miezi mitano, na pia hutumia za madukani aina ya NPK.

Baada ya kuliandaa shamba vyema, mkulima huyo huipanda miche kwa kuacha nafasi ya mita 3 na mita 2 mtawalia, kutoka kwa mmea mmoja hadi kwa mwingine.Mkulima huyo huchuma kilo 130-160 kila baada ya wiki mbili kutoka kwa mimea 140.

“Huuza mazao yangu kwa wafanyabiashara wanaonunua kutoka kwa shamba na kusafirisha na kuuza jijini Nairobi. Bei ni Sh60 kwa wateja wa hapa nyumbani na Sh100 kwa wateja wanaouzia Nairobi.Mbali na mikarakara, Sawe pia hukuza mimea ya viungo aina ya rosemary.

“Kwa sasa, nina miche ya rosemary zaidi ya 4,000 na huwauzia wakulima wengine,” asema, akiongeza kuwa, mmea huo husaidia kuwazuia wadudu kuvamia mimea shambani.

“Kwa wakati huu hawezi kutosheleza soko kwa mazao yake; wakati mwingine inabidi nikatize baadhi ya oda kwa sababu siwezi kuzalisha (makarakara) ya kutosha,” asema, akiongeza kuwa, ana wateja sita wanaong’ang’ania matunda yake.

“Yeyote anayenuia kujitosa katika ukuzaji wa mikarakara asifikirie mara mbili kwa sababu tutakapoingia katika shughuli ya kuongeza thamani, tutahitaji matunda mengi kuliko yale tunayozalisha.” asema, akiongeza kuwa, ukuzaji wa mikarakara ni mojawapo ya shughuli zinazohitaji mtaji usiokuwa mwingi na huwa na faida tele.

Mkulima huyo anafichua kuwa, anapania kujitosa katika shughuli ya kuongeza thamani kwa matunda anayoyazalisha kwa kutengeneza sharubati.

Aidha, anapania kulipanua shamba la ukuzaji ili awe na matunda mengi.

  • Tags

You can share this post!

Uhaba wa maji mateso tele kwa wakazi vijijini

UJASIRIAMALI: Msanifu stadi, kazi ameweka blockcheni

T L