Makali ya janga la ukame yawasukuma baadhi ya wanaume kutupa familia

Makali ya janga la ukame yawasukuma baadhi ya wanaume kutupa familia

Na KALUME KAZUNGU

WANAWAKE katika baadhi ya vijiji vya Kaunti ya Lamu, wamelalamikia jinsi waume wao walivyotoroka na kuacha familia zao zikitaabika wakati wa janga la ukame.

Hali hiyo imelazimu wanawake na watoto kuachwa ukiwa, wengine, hasa akina mama wakilazimika kufanya kazi za vijungu jiko ili kukimu familia zao.Baadhi ya vijiji ambavyo Taifa Leo ilizuru na kubaini kwamba wanaume wamehama ni Kiangwe, Mangai, Mararani, Milimani, Pandanguo, Shee Mgambo, Maisha Masha, Katsaka Kairu, Moa na Dide Waride.

Vijiji hivyo ndivyo vilivyoathiriwa zaidi na ukame na kulazimu mamia ya mifugo kufariki kwa kukosa maji na lishe.Wakazi wengi kwenye vijiji hivyo pia wamedhoofika kiafya, wengi wao wakiwa wamekonda, dhihirisho tosha kwamba njaa na kiu ya maji inawatesa.Ijapokuwa katika maeneo mengine kuna wanaume na vijana ambao huhama pamoja na mifugo ili kuwatafutia mifugo lishe na maji, imebainika kwamba kuna wale walioondoka nyumbani bila sababu mwafaka na kufikia sasa hawajulikani waliko.

Katika kijiji cha Kiangwe ambacho kiko ndani ya msitu wa Boni, Taifa Leo ilikutana na Bi Maryam (tumebana jina lake kamili kuepushia familia yake fedheha), ambaye alidai kuwa mumewe aliondoka nyumbani zaidi ya miezi minne iliyopita.Mama huyo mwenye umri wa miaka 24 ana watoto wanne, kitindamimba akiwa na umri wa miaka miwili.

Mara ya kwanza mumewe alipoondoka nyumbani, Maryam anasema alikuwa akimpigia simu mara kwa mara na kumpa moyo kwamba alikuwa akitafuta vibarua ili kukimu familia yao baadaye akawa mteja.?“Baadaye alianza kuongea kwa ukali, akidai ameshindwa kabisa kukimu familia yake.

Mwishowe alinifungia simu na hadi wa leo sijui aliko,” akasema.?Kulingana naye, anashuku tabia hizo za mumewe ni kusudi kujaribu kukwepa majukumu ya ulezi wakati huu ambapo gharama ya maisha imepanda na ukame umesababisha ukosefu wa chakula cha kutosha.?“Vibarua hakuna.

Mimi mwenyewe nimeanza kushindwa kukimu hawa watoto. Mara nyingi tunalala njaa. Nigeomba serikali kunikumbuka kwa msaada wa chakula, maji na pia kumtafuta mume wangu ili tusaidiane haya malezi ya watoto wetu wadogo,” akasema Bi Tindi.?Katika kijiji cha Shee Mgambo kilichoko tarafa ya Hindi, Bi Kache ni miongoni mwa wanawake ambao hawajui mahali mabwana zao walitorokea wakati ukame ulipoanza kukeketa jamii za eneo hilo.

Mwanamke huyo, 35, anasema ni mwezi wa pili sasa tangu mumewe alipohama nyumbani akidai kwenda kutafutia familia hiyo chakula.?Familia hiyo imeajaliwa watoto sita, wengine wakiwa ni wanafunzi wa shule ya msingi.?Anasema licha ya simu ya mumewe kuwa wazi, hajawahi kumpokelea simu yake kila anapotafutwa.?“Alipokea simu tu siku moja, karibu mwezi mmoja uliopita na kudai kuwa hali ni ngumu kwani hajapata kibarua chochote.

Alisema eti yuko kisiwani Lamu. Tangu hapo hajawahi kunipokelea simu tena,” akasema.?Katika kijiji cha Maisha Masha, Bi Sidi pia alilalamika kuwa mumewe ambaye ni fundi wa kujenga alitoroka nyumbani tangu miezi sita iliyopita na hajakuwa akimsaidia katika malezi ya watoto wao watatu.

Alieleza kuwa, hali imekuwa ngumu kwani jitihada zake za kujaribu kilimo ziligonga mwamba mwaka huu kutokana na ukame unaoendelea.?Anasema tumaini lake kwa sasa ni mumewe arudi nyumbani ili kumsaidia kukimu mahitaji ya familia yao.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo pia ulibaini kuwa wazee wa mitaa tayari walikuwa wamefanya vikao mbalimbali na kuafikiana kuchukua orodha ya majina ya wanaume wote wanaodaiwa waliotoroka taabu za ukame ili mipango ifanywe kuwatafuta warudi kutunza familia zao.

You can share this post!

Mama Ida tumaini tele Raila atashinda kura

PETER NGARE: Tusihadaike eti ‘kazi ni kazi’ wala pesa...

F M