Makamishna na wakuu wenye kibarua uchaguzi ukifanyika

Makamishna na wakuu wenye kibarua uchaguzi ukifanyika

NA CECIL ODONGO

WAKENYA wakipanga foleni leo Jumanne kushiriki katika Uchaguzi Mkuu, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC), Wafula Chebukati na makamishina wenzake pamoja na wafanyakazi wa tume hiyo ndio wanaotarajiwa kutekeleza wajibu muhimu kutangaza matokeo ya Urais.

Kando na Bw Chebukati, makamishna wengine wa IEBC ni Boya Mulu, Abdi Guliye ambao walihudumia tume kwenye uchaguzi wa 2017. Wengine Francis Wanderi, Juliana Cherera, Irene Cherop na Justus Abonyo pia watasimamia uchaguzi huo baada ya kuchukua nafasi za Dkt Roselyn Akombe Kwamboka, Consolata Nkatha Bucha Maina, Dkt Paul Kibiwott Kurgat na Margaret Wanjala Mwachanya ambao walijiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Wafula Chebukati

Bw Chebukati alizaliwa mnamo 1961 katika Kaunti ya Bungoma, Magharibi mwa nchi.Bw Chebukati ambaye boma lake lipo katika eneobunge la Kiminini, Kaunti ya Trans Nzoia, alisomea Shule za upili za St Peters Mumias, Bokoli na Lenana High.

Ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na pia stashahada kutoka Chuo cha Sheria (KSL).

Amehudumu kama mwenyekiti wa IEBC kuanzia Januari 18, 2017 na muda wake wa miaka sita unatamatika mnamo Januari 2023. Pia aliwania kiti cha ubunge kwa kutumia tikiti ya chama ODM katika eneobunge la Kiminini mnamo 2007 lakini akashindwa.

Amehudumu katika taaluma ya uanasheria kwa zaidi ya miaka 36 na Wakenya wanasubiri kuona jinsi ambavyo ataendesha uchaguzi huu baada ya kukashifiwa mnamo 2017 kutokana na hatua ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa Urais.

Bi Juliana Cherera

Alichaguliwa na makamishina wenzake kama Naibu Mwenyekiti wa IEBC mnamo Septemba 2021, akichukua nafasi ya Catherine Nkatha aliyejiuzulu.

Kwa wakati mmoja alikuwa mwalimu wa shule ya msingi ya Mvita katika Kaunti ya Mombasa. Ana shahada ya ualimu – Kiswahili na Jiografia, shahada ya uzamili katika elimu, usimamizi na uongozi pamoja na stashahada katika usimamizi wa miradi.

Naibu Mwenyekiti wa IEBC, Bi Juliana Cherera. PICHA | MAKTABA

Mnamo 2015, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alimteua kama Afisa Mkuu wa Elimu katika kaunti hiyo. Atakuwa akisimamia uchaguzi wake wa kwanza kama kamishna na naibu mwenyekiti wa IEBC.

Katika tume hiyo yeye ni mwenyekiti wa kamati inayosimamia uhamasisho na elimu kwa wapigakura.

Bw Boya Molu

Alizaliwa katika Kaunti ya Marsabit mnamo 1978.Bw Mulu alisomea usimamizi wa kibiashara na pia ana stashahada ya usimamizi wa wafanyakazi kutoka KNEC. Ana tajiriba ya zaidi ya miaka 15 katika usimamizi wa mashauri ya wafanyakazi.

Kabla ya kujiunga na IEBC, alihudumu katika nyadhifa mbalimbali zinazohusiana na mashauri ya wafanyakazi katika Benki Kuu ya Kenya (CBK) na pia Idara ya Mahakama.

Atakuwa akisimamia uchaguzi mkuu kwa mara ya pili kwa sababu alikuwa miongoni mwa makamishina waliohudumu kwenye IEBC katika kura ya 2017.

Profesa Abdi Guliye

Profesa Guliye alizaliwa katika Kaunti ya Wajir mnamo 1962.

Ana shahada ya uzamifu kutoka Chuo Kikuu cha Egerton ambapo alijikita katika masuala ya kilimo. Pia ana shahada ya uzamifu kutoka Taasisi ya Rowet na Chuo Kikuu cha Aberdeen (Scotland, Uingereza).

Wakati alipokuwa akituma maombi ya kusaka kazi ya IEBC, alijitetea kuwa angetumia weledi na tajiriba yake aliyotumia kusimamia uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi, kuhakikisha kuna uwazi na kuepusha ghasia.

Profesa Abdi Guliye. PICHA | MAKTABA

Pia alikuwa kamishna wakati ambapo uchaguzi mkuu uliandaliwa nchini 2017.

Ni kati ya makamishna ambao kandarasi zao kwenye tume hiyo zitakuwa zikitamatika mwaka 2023.

Prof Guliye ana tajriba ya kufundisha katika vyuo vikuu mbalimbali kwa zaidi ya miaka 27 na pia alihudumu kwenye bodi ya mashirika mbalimbali kabla ya kupewa kazi IEBC.

Bw Francis Wanderi

Pia ni kamishna ambaye alipata kazi IEBC mnamo Septemba mwaka jana baada ya kuhojiwa na kamati ya bunge. Ana shahada ya digrii katika elimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na pia shahada ya uzamili ya Sayansi kutoka Boston, Marekani.

Kabla ya kujiunga na tume, Bw Wanderi alikuwa mwenyekiti wa Shirika la Kustawisha Viwanda Nchini (EPZ) na pia mkurugenzi wa Kamati ya Roots Credit.Ana uzoefu wa kusimamia mashirika ya umma na mengine ya kibinafsi ambayo yanajikita sana katika uvumbuzi. Amejihusisha na usimamizi kwa zaidi ya miaka 32.

Kwenye tume, anasimamia kamati ya fedha na usambazaji.

Bw Justus Nyang’aya

Bw Nyang’aya aliwahi kuhudumu kama mkurugenzi wa shirika la Kimataifa la Amnesty. Shirika hilo hupigania watu wanaotimuliwa kwa lazima, na pia haki za akina mama na watoto.

Ana shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha London na ni mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia. Kabla ya kujiunga na IEBC, alikuwa mkurugenzi wa Shirika la Lead Africa.

Bi Irene Masit

Bi Masit ana uzoefu wa kufanya kazi kwa miaka 25 katika mashirika yasiyo ya kiserikali na ya serikali.

Ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi na Uwazi katika tume hiyo. Kabla ya kutua IEBC mwaka 2021, alikuwa akihudumu katika Bodi ya Kitaifa ya Hazina ya Kifedha ya Maeneobunge (IEBC).

Bi Masit ana shahada ya usimamizi wa wafanyakazi kutoka Chuo Kikuu cha Manchester na pia ana ujuzi na uzoefu kuhusu masuala ya kifedha, uongozi na usimamizi wa kibiashara.Atakuwa akisimamia uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza.

Bw Michael Ouma

Ndiye Mkurugenzi wa masuala ya teknolojia na mawasiliano na ambaye alichukua nafasi ya Bw Chris Msando aliyeuawa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Ouma ana uzoefu wa miaka 20 katika masuala ya teknolojia na pia miaka mingine 10 kwa kutumia teknolojia kusimamia uchaguzi.

Kimasomo, ana shahada ya uzamili katika masuala ya biashara kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.Kazi yake kuu ni kuhakikisha kuwa matokeo yanasambazwa kwa njia ya kiteknolojia kwenye kura za Urais.

Bw Marjan Hussein

Bw Hussein aliteuliwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC mnamo 2018 kufuatia kutimuliwa kwa Ezra Chiloba mnamo Oktoba 2018.

Bw Hussein ni mhasibu na pia mkaguzi wa vitabu vya hesabu. Ana shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. Kazi yake kuu katika uchaguzi wa leo Jumanne ni kusimamia afisi kuu ya tume hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Mamilioni ya Wakenya washiriki uchaguzi leo

Mlima Kenya njia panda katika uchaguzi wa leo Agosti 9

T L