Habari Mseto

Makamishna wa usalama waongezewa mamlaka

January 23rd, 2019 1 min read

Na MOHAMED AHMED

RAIS UHURU Kenyatta Jumanne aliwapa makamishna wa kanda nguvu zaidi kama walizokuwa nazo kabla ya kabla ya kubadilishwa kwa Katiba.

Washirikishi hao wa mikoa na makamishna wa kaunti sasa watakuwa ndio wakuu wa vitengo kadhaa vya shughuli za serikali na pia masikio na macho ya serikali kuu mashinani.

Rais Kenyatta aliwaambia washirikishi hao wa mikoa na kaunti kuwa watakuwa “wenye mamlaka” ya kusimamia miradi ya serikali na shughuli za kiusalama.

Hali hii inalingana na ile ya wakati wa utawala wa rais mstaafu Daniel Moi, ambapo wakuu wa mikoa na wilaya almaarufu PC na DC mtawalia walikuwa na madaraka makuu yaliyorithiwa kutoka utawala wa wakoloni

Miongoni mwa nguvu walizopewa maafisa hao ni pamoja na fursa ya kusimamia kamati kadhaa ambazo rais alisema kuwa ni hatua ambayo itasaidia kuhudumia Wakenya na kuhakikisha kuwa mali ya umma inalindwa.

Rais Kenyatta alisema kuwa wakuu hao pia watatarajiwa kupambana na ufisadi na kuwataka kuonyesha ujasiri wa kupigana nao. Maafisa hao pia watahitajika kuhusika pakubwa katika kufanikisha Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

“Ni matarajio yangu kuwa mtakuwa mkipeana ripoti kwangu kuhusiana na kutekelezwa kwa ajenda hizi, na kueleza shida zozote kuzihusu, pamoja na kueleza umuhimu wake mashinani kwa wananchi,” akasema rais.

Alisema kuwa maafisa hao pia watakuwa wakuu wa kamati za mazingira na maji katika maeneo yao ya kuhudumu: “Mtakuwa na maswali ya kujibu iwapo kutakuwa na kesi zozote za uharibifu wa mazingira. Ni lazima tulinde mazingira yetu kwa ajili ya kizazi chetu kijacho.”

Aliwataka maafisa hao kushirikiana na serikali za kaunti.