HabariSiasa

Makamishna wamtoroka Chebukati wakisema ameshindwa na kazi

April 16th, 2018 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati Jumatatu ametorokwa na makamishna watatu wa tume hiyo.

Makamishna hao, Margaret Mwachanya, Connie Maina na Paul Kurgat wamejiuzulu wakidai kuwa Bw Chebukati hana uongozi unaofaa.

Hata hivyo, kujiuzulu kwao kunaonekana kuchangiwa zaidi na hatua ya Chebukati kumpa likizo ya lazima Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba, anayetuhumiwa kufuja pesa za mwananchi wakati wa utoaji kandarasi za kununua vifaa vya uchaguzi, na pia kuwalipa mawakili mamilioni bila kufuata utaratibu.

Chiloba alikuwa ameenda kortini kupinga hatua hiyo ya kumsimamisha kazi, lakini Mahakama inayoshughulikia kesi baina ya mwajiri na mfanyikazi, ilikubaliana na Chebukati kwamba lazima Chiloba aende likizo ili asiingilie uchunguzi.

Katika taarfia iliyotolewa na Bi Mwachanya, makamishana hao watatu wamesema tume hiyo imegeuzwa chumba cha kubuni taarifa za uongo, ukosefu wa uaminifu na uwanja wa kudunisha makamishana wachapa kazi, hali ambayo imelemaza utendakazi wa tume nzima.

“Kwa muda mrefu sasa, na kwa nyakati nyingi, mwenyekiti wa tume hii ameshindwa kuendesha jahazi wakati linayumbishwa na mawimbi, almelemewa kutoa mwongozo katika nyakati ngumu,” watatu hao wamesema.