Habari Mseto

Kondakta akiri kuiba gunia la omena

October 19th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KONDAKTA wa matatu zinazohudumu barabara ya Kawangware alishtakiwa Alhamisi kwa kuiba gunia la samaki aina ya omena wenye thamani ya Sh14,000.

Na wakati huo huo mfanyabiashara na kibarua wake walishtakiwa kwa kumnyang’anya kimabavu mwanakandarasi wa kaunti ya Taita Taveta Sh732,000 na kumrusha kutoka kwa gari ikiwa kasi.

Kondakta huyo Ronard Moenga Basweti alikiri mbele ya hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani kuwa aliiba gunia la omena ya Bi Saoke Lago.

Alikiri aliiba samaki hao mnamo Oktoba 16 katika eneo la kuegesha magari ya matatu ya  Kenya Railways. Aliomba msamaha na kusema ameghairi matendo yake.

Mahakama iliamuru afisa wa urekebishaji amhoji Bw Basweti kabla ya kuhukumiwa.

Mshtakiwa atarudishwa tena mahakamani Novemba 6, 2018 afisa wa urekebishaji tabia awasilishe ripoti kumuhusu mshtakiwa.

Katika kisa hicho cha wizi wa mabavu Bw Sameer Abdulaziz Kassim (pichani) na Peter Kavoi Musili almaarufu Alphonse Mutuku walikanusha shtaka la kumnyang’anya Bw Amos Charo Saru mnamo Oktoba 17 2018 Sh732,000.

Washtakiwa walidaiwa walimhandaa Bw Charo anayehudumu  mjini Voi asafiri hadi Nairobi ndipo wamwonyeshe mahala pa kununua vifaa vya mjengo  viko bei rahisi.

Mabw Kassim na Musili walimtaka Bw Charo abebe pesa tasilimu za kununua vifaa vya mjengo.

Mahakama ilielezwa washtakiwa walimzungusha mlalamishi kwenye maduka kadhaa na hatimaye wakamtaka aingie kwenye gari wakavinunue fito vya chuma.

Mlalamishi alifurushwa nje ya gari ikiwa kasi. Aliokolewa na msamaria mwema akiwa na majeraha na kupelekwa hospitali na hatimaye akaripoti kwa Polisi.

Polisi waliwapata washtakiwa na Sh400,000.Washtakiwa walikana shtaka na kuomba waachiliwe kwa dhamana.

Bi Onkwani aliwaachilia kwa dhamana ya Sh3 milioni. Kesi itasikizwa Novemba 22, 2018.