Habari Mseto

Makanisa Kiambu yajiandaa vilivyo kuwapokea waumini

July 18th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

HUKU Covid-19 ikizidi kusambaa nchini, makanisa yanaendelea kujizatiti kuona ya kwamba yanajipanga kupokea waumini kwa maombi.

Kasisi wa kanisa katoliki la St Francis mjini Ruiru Bw Charles Njoroge, alisema wanajipanga kuwa na ibada sita kwa siku mbili.

“Tutaanza na ibada ya kwanza mnamo Jumamosi jioni halafu Jumapili tutakuwa na ibada zingine tano ili kutosheleza mahitaji ya waumini kadhaa,” alisema Kasisi Njoroge.

Alisema hata ingawa wamepanga hivyo, bado kuna washirika wengi ambao watakosa kupata nafasi ya kuhudhuria ibada ya Jumapili.

Bw Stanley Ngure wa Kanisa la Deliverance Church mjini Juja anasema watafanya juhudi kufanikisha awamu tatu za ibada mnamo Jumapili.

Alisema bado wako na changamoto katika juhudi zao za kupanga ratiba hiyo.

“Hata ingawa mambo ni magumu kufuatia janga la Covid-19, tutajaribu kadri ya uwezo wetu ili kuwapa washirika wetu chakula cha kiroho,” alisema mchungaji Ngure.

Serikali ilitoa mwongozo ya kwamba waumini wasiozidi 100 ndio watakubaliwa kushiriki katika maombi kanisani.

Hata hivyo, wachungaji wengi wanaendelea kulalamika wakisema ya kwamba hatua hiyo ya serikali haitawafaa kama wachungaji.

Wanazidi kudai ya kwamba waumini wengi watakosa kumuabudu Mungu kama walivyozoea hapo awali.

Serikali bado imeweka vikwazo kwa wazee wa umri wa zaidi ya miaka 58 na zaidi na watoto wa umri wa miaka 13 kwenda chini ikiwakataza kuhudhuria ibada kanisani ili kuzuia maambukizi ya Covid-19.

Hata hivyo, swali nzito ni jinsi wachungaji watakavyowateua waumini wao 100 na kuwaacha wale wengine kuwa nje ya kanisa.