Habari Mseto

Makanisa na misikiti kufunguliwa Julai 14

July 8th, 2020 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MAENEO ya ibada sasa yatafuguliwa kuanzia Jumanne Julai 14, 2020 chini ya masharti makali ya kuwakinga waumini dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

Akitoa tangazo hilo Jumanne kwenye kikao na wanahabari katika jumba la Ufungamanom, Nairobi, mwenyekiti wa Baraza la Viongozi wa Kidini kuhusu Covid-19 Askofu Mkuu Anthony Muheria alisema itakuwa ni wajibu wa wakuu wa makanisa husika kuhakikisha masharti hayo yanazingatiwam na waumini.

“Kufunguliwa kwa sehemu hizo za ibada kutafanywa kwa awamu nne kulingana na hali ya maambukizi itakavyokuwa sawia na jinsi masharti yaliyowekwa yatafuatwa” akasema Askofu Muheria ambaye ni kiongozi wa Kanisa Katoliki jimbo la Nyeri.

Alikariri kuwa katika awamu hii ya kwanza, ni waumini 100 pekee wataruhusiwa katika ibada kila ibada. Vile vile, watoto wasiozidi umri wa miaka 13 na wazee wenye umri wa miaka 58 hawataruhiwa kuhudhutia ibada hizo.

“Kama Rais Kenyatta alivyosema jana (Jumatatu) itakuwa wajibu wa kila mmoja wetu kama viongozi wa kidini, waumini na wananchi kwa ujumla kufuata masharti yaliyowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Wizara ya Afya,” akasema Askofu Mkuu Muheria ambaye alikuwa ameandamana na wanachama wengine wa baraza hilo.

Kwa muhtasari masharti ya kufungua sehemu hizo za ibada yaliyotangazwa na baraza hilo yanajumuisha:

  • · Kuhakikisha kila eneo la ibada liwe na eneo la kuosha mikono kwa sabuni na maji ya kutiririka
  • · Kuvalia barakoa kila wakati ndani na nje ya majumba ya ibada
  • · Kuweka umbali wa mita 1.5 kutoka mtu mmoja hadi mwingine
  • · Ibada isizidi watu zaidi ya 100
  • · Walio chini ya miaka 13 na walio zaidi ya miaka 58 hawataruhusiwa kwa ibada
  • · Kila ibada kuchukua saa moja lakini idadi ya ibada zinaweza kuwa zaidi ya moja
  • · Sehemu za ibada zisafishwe kila wakati
  • · Vipima joto vitumiwe

Kwa mara nyingine Askofu Muheria amewasihi waumini kufuatilia kikamilifu masharti hayo ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Covid-19.

“Tunaelewa hamu iliyoko ya kurejea katika sehemu za ibada lakini tunapaswa kujiandaa vilivyo kwa kuweka mikakati ya kujikinga hadi wakati ambapo tutajumuika tena katika sehemu zetu za ibada kama zamani,” alisema Muheria.

Kwa mujibu wa Muheria,kamati za dini mbalimbali zitabuniwa katika kaunti na kaunti ndogo ili kufanikisha utekelezaji wa masharti hayo.

Aidha baraza hilo lilipendekeza kubuniwa kwa kamati ya kushughulikia covid-19 katika kila sehemu ya ibada.