Makanisa yachomwa, ukuta wapakwa kinyesi Kisii

Makanisa yachomwa, ukuta wapakwa kinyesi Kisii

Na SAMMY WAWERU

Wakazi wa kijiji cha Otambu, Kisii ya Kati, Kaunti ya Kisii wameendelea kuzongwa na maswali chungu nzima kufuatia kisa ambapo makanisa matatu eneo hilo yalichomwa usiku.

Kulingana na wenyeji, mnamo Ijumaa asubuhi waliamkia kushangazwa na tukio la makanisa hayo kuchomwa kihuni katika hali isiyoeleweka na watu wasiojulikana.

Ukuta wa kanisa moja na ambalo halikuchomeka sana nao ulipakwa kinyesi cha binadamu, jambo ambalo limesababisha wakazi wa kijiji hicho kupigwa na mshangao.

Kwenye mahojiano, walisema hawajawahi kushuhudia visa vya aina hiyo.

Naibu chifu wa eneo hilo, Bw Tadias Omosa hata hivyo amewahimiza kuwa na utulivu ili kuruhusu uchunguzi kufanyika.

Bw Omosa pia amewataka kushirikiana na maafisa wa polisi ili kusaidia kutambua wahuni waliotekeleza kisa hicho.

“Ninawahimiza wajitathmini na waangalie wanaoishi nao eneo hilo, kujua iwapo wameingiliwa na shetani kwa sababu watu wengi walisema ni kitendo cha kishetani,” Bw Omosa alisema.

Wizi wa vifaa vya thamani vya makanisa hayo hata hivyo haukuripotiwa, mabati ya paa yaliyong’olewa yakionekana kusalia.

Uchunguzi wa kitendo hicho umeanzishwa.

You can share this post!

Tapeli mkubwa wa Showbiz Wilkins Fadhili acheza kama yeye...

BBI: SAINI ZA UHURU, RAILA ZATUPWA