Makanisa yaililia serikali kuyaruhusu kuandaa kesha za Mwaka Mpya

Makanisa yaililia serikali kuyaruhusu kuandaa kesha za Mwaka Mpya

TITUS OMINDE na OSCAR KAKAI

VIONGOZI wa kidini wanataka serikali kuondoa kafyu ili wapate nafasi ya kushiriki maombi ya mkesha wa mwaka mpya usiku wa kuamkia Januari 1, 2021.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa shirikisho la wahubiri wa Uasin Gishu, Kasisi Boniface Simani, walisema serikali inapaswa kuwaruhusu Wakristo kufanya maombi ya Mwaka Mpya ili kutakasa mwaka wa 2021.

“Kama viongozi wa kiroho tunahitaji kuruhusiwa kuwa na sala za usiku ili tutakase nchi kutokana na majanga ambayo yameshuhudiwa mwaka huu kabla ya Mwaka Mpya wa 2021,’ alisema Bw Simani.

Makasisi hao walisema maombi ya mkesha wa mwaka ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo taifa la Kenya linapopitia changamoto nyingi kutokana na virusi vya corona, uvamizi wa nzige, ajali, usalama wa wanafunzi kabla ya kufunguliwa kwa shule Januari miongoni mwa masuala mengine tata.

Wakihutubu mjini Eldoret, walimsihi Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto kutimiza ombi lao na kuungana na Wakenya kusali.

Askofu Wilson Kurui wa kanisa la Jesus Love alisema nafasi ya kushiriki katika ibada ya mkesha wa mwaka mpya ni muhimu sana kwa taifa kabla ya mwaka wa 2021 na serikali inapaswa kuwapa nafasi.

“Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanapaswa kuzingatia wito wetu na kuungana na Wakristo wengine na kutii wito huo na kushiriki katika sala,” alisema Bw Kurui.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Ayub Ali amewaonya wakazi dhidi ya kukiuka sheria za kukabiliana na maambukizi ya corona hasa msimu huu wa sikukuu.

Bw Ali alisema polisi wako katika tahadhari ya kuwakamata wakazi wote wanaopatikana wakikiuka maagizo ya kutotoka nje na kutozingatia sheria za kukabiliana na Covid-19.

Kwingineko, wakazi na wafanyabiashara wa vilabu vya kuuza pombe katika mji wa Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi, wameonywa dhidi ya kuuza pombe wakati wa kafyuu.

Akitoa onyo hilo jana mjini Kapenguria, Kamanda wa Polisi katika Kaunti hiyo, alisema wakazi wengi wa eneo hilo wanakunywa pombe kiholela.Bw Tumwet alisema wenye vilabu ambao watapatikana wakiuza pombe saa ambazo hazistahili watachukuliwa hatua kali.

“Ukipatikana ndani ya kilabu wakati usiofaa utakamatwa na kushtakiwa na hatutakuwa na msamaha kwa yeyote,” akasema. Bw Tumwet alisema maafisa wa polisi watafanya msako kila mahali na kuhakikisha kuwa hakuna anayetengeneza na kuuza pombe haramu.

Afisa huyo alitaja kitongoji duni cha Mathare mjini humo kama eneo ambalo pombe haramu inauzwa kwa wingi.“Kuna watu wanasahau majukumu yao ya nyumbani sababu wamepotelea kwenye ulevi,” alisema.

You can share this post!

Bara la Afrika lalala huku dunia ikianzisha chanjo ya corona

Wanafunzi wengi zaidi kusomea chini ya miti 2021