Makanisa yamtaka Raila azime maandamano aliyotangaza yatafanyika

Makanisa yamtaka Raila azime maandamano aliyotangaza yatafanyika

NA SAMMY KIMATU

KUNDI moja la viongozi wa kanisa limeomba kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw Raila Odinga kusitisha maandamo yaliyopangwa na pia kumrai asiandae mkutano Jamhuri Dei.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Askofu Dkt Josphat Njoroge, Sauti Mashinani Gospel Ministers Movement (SMGMM) walisema maandamano hayo yakifanyika, yatasabisha umwagikaji wa damu.

Isitoshe, kundi hilo la wahubiri wa makanisa mbalimbali katika kaunti ya Nairobi walisema maandamano hayo yatairudisha nchi ya Kenya nyuma kimaendeleo.

“Maandamano yataturudisha Kenya nyuma na kusabaratisha uchumi huku wahalifu wakitumia fursa hiyo kupora mali ya watu waliyotafuta kwa jasho lao,” akasema Dkt Njoroge.

Aidha, Dkt Njoroge alisema badala yake, wameshauri Bw Odinga kufanya kikao cha mazungumzo na Rais William Ruto kwa faida ya Kenya.

“Kenya ni kubwa kuliko viongozi hawa wawili. Kuna umuhimu wa Bw Raila kuzungumza na Rais Ruto na kumwambia kule angependa kuangaziwe ili Kenya ipate kusonga mbele kimaendeleo badala ya kuambia wakenya waandamane barabarani,” Dkt Njoroge akasema.

Dkt Njoroge ambaye kadhalika ni kinara wa kanisa la Jubilee Restoration Christian Church alizunguma wikiendi katika mkutano na wanachama wa kundi hilo.

Hafla hiyo ilifanyika katika kanisa la JRCC, Njiru kaunti ya Nairobi.

Akiongoa na Taifa Leo, Dkt Njoroge alisema lengo kuu la kundi hilo ni kuwatetea viongozi wenzao wa makanisa ambao makanisa yao yalikwama na mengine kufungwa kufuatia janga la Corona.

Bali na hayo, kundi hilo lilitoa msaada wa chakula kwa familia zilizokumbwa na njaa katika kijiji cha Orini, Kajiado Kati kwenye kaunti ya Kajiado.

Waathiriwa wa njaa katika eneo hilo, kwa mujibu wa Dkt Njoroge walitembea kilomita 25 kutoka makwao kufika kituo cha kugawa mlo.

“Familia zaidi ya 200 walipata chakula cha msaada kutoka kwa makanisa yetu kuwalenga wakenya walio na mahitaji ya chakula kufuatia kiangazi kilichokithiri kwa muda mrefu katika baadhi za kaunti za Kenya. Tunawarai wenzetu makanisani wachange chochote walicho nacho ili tuwasaidie ndugu zetu wakenya. Hatutaki kama kanisa kusikia mkenya yeyote amefariki kutokana na njaa,” Bw Njoroge akasema.

Wahisani hao waligawa chakula ikiwemo mchele, unga, mahindi na mafuta pamoja na manguo kwa watu kadhaa.

Bali na Kajiado, wahubiri hao wameratibu kuzuru kaunti nyingine kuwagawia chakula waathiriwa wa njaa.

Vilevile, wameongoza makundi mengine katika kampeni ya kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.

“Tunapiga kampeni ya kupanda miti ndiposa tunawashauri wakenya kujitolea katika upanzi wa miti ili kukabili changamoto za tabianchi. Miti ikipandwa kwa wingi, tutapata mvua ya kutosha na kila kitu kitakuwa shwari,” Dkt Njoroge asema.

Wanachama hao wameomba wizara ya ardhi, idara ya misitu na Idara ya Masuala ya Mazingira kutoa ushauri kwa wakenya ni miti ipi inastahili kupandwa ili kuepuka upanzi wa miti inayokausha vyanzo vya maji.

“Sio bora kupanda miti ila muhimu hapa ni kupanda miti bora itakayochangia kuvuta mvua na kuboresha mazingira,” Kiongozi Njoroge akaambia wanahabari.

skimatu@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud avunja rekodi ya Thierry...

TALANTA: Dogo mkali wa tenisi

T L