Habari Mseto

Makanisa yapeperushe ibada mitandaoni lakini yazingatie sheria – Mahakama

April 26th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

Mahakama kuu imeruhusu makanisa kutangaza ibada zao kupitia televisheni, redio au mitandao mingine bila kuvunja mikakati iliyowekwa na Serikali kuthibiti ugonjwa wa corona.

“Agizo hili lisichukuliwe kuwa idhini ya kuruhusu makanisa kufanya mikutano ya ibada kila jumapili kinyume na mikakati iliyowekwa na Serikali,” alifafanua Jaji James Makau.

Pia Jaji Makau aliruhusu ibada zitangazwe katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Zoom na YouTube.

Jaji Makau aliamuru wahubiri wazingatie sheria na masharti yaliyowekwa na Serikali kuhakikisha maradhi ya Corona yameangamizwa..

Jaji Makau alitoa maagizo hayo katika kesi iliyowasilishwa na Mabw Don Mutugi Manjau , Joan Miriti na Alex Gichunge walioomba korti iamuru Waziri wa usalama Dkt Fred Matiang’i , Waziri wa Afya Mutahi Kagwe. Waziri wa Habari na Teknolojia Bw Mucheru , Mwanasheria Mkuu na Inspekta Jenerali Nicholas Mutyambai waruhusu ibada zipeperushwe na vituo vya televisheni siku zilizotengwa.

Watatu hao walitaka kila dhehebu litengewe siku muafaka za kuwatangazia jumbe za mahubiri waumini wao kupitia televisheni bila kusumbuliwa na polisi.

Pia waliomba mahakama wenye kupeperushwa mahubiri wa vituo vya televisheni wasivurugwe na polisi.

Walalamishi waliomba viongozi na waumini wachache wakubaliwe kuhudhuria ibada upeperushaji huo ukiendelea.

Katika uamuzi wake Jaji Makau aliruhusu mahubiri yatangazwe katika tuvuti na mitandao ya kijamii na katkka runinga.

Aliwaamuru walalamishi wakabidhi idara walizoshtaki hati za kesi katika muda wa siku saba.

Kesi itasikizwa Mei 5,2020.