Makanisa yataka adhabu ya kiboko irudishwe shuleni

Makanisa yataka adhabu ya kiboko irudishwe shuleni

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI wa makanisa ya Kievanjelisti na Kiasili (FEI CCK), kutoka Kiambu na Nairobi, sasa wanaitaka serikali irejeshe adhabu ya kiboko shuleni.

Wakiongozwa na Askofu mkuu wa Glory Outreach Assembly (GOA) Kahawa Wendani, Bw David Munyiri, wachungaji hao wanasema ni kiboko tu kitakachorejesha kwa haraka nidhamu ya wanafunzi.

‘Tunajua wengi hawatapenda msimamo huu lakini ni sharti amri ya kudumu itekelezwe kwa wanafunzi hao,’ alisema Bw Munyiri.Aliwashauri wazazi wawe mstari wa mbele kuwashauri wana wao kabla ya kupeleka matakwa ya nidhamu kushughulikiwa na mwalimu.

Alieleza kuwa malimbikizi ya masomo, maswala ya covid- 19, na kukaribia kwa mitihani, ni baadhi ya mambo yanayowatia wanafunzi kiwewe, akisema serikali iingilie kati kwa haraka.Alieleza kuwa kama wachungaji wanajiandaa kuzuru shule kadha kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu kudumisha nidhamu na kujali maisha yao ya baadaye.

Wachungaji hao walikashifu tabia ya wanasiasa kuwapa vijana kiinua mgongo ( hela chache), jambo wanayodai vijana hao huzinunulia dawa za kulevya na pombe.Waliwashauri wazazi pia kuwajibika hasa wakati huu wanafunzi wamerejea nyumbani kwa likizo fupi.

‘ Huu ni wakati wa wazazi hao kuketi chini wa wana wao na kuwashauri kwa kina umuhimu wa masomo na maisha yao ya baadaye,’ alifafanua Bw Munyiri.

Walimu pia walishauriwa kufuatilia mienendo kamili ya wanafunzi na hatua kali kuchukuliwa dhidi yao bila kuwadekeza.

You can share this post!

Mbunge ajitetea kuhusu matumizi ya fedha za NG-CDF

Washukiwa wa wizi wa mabomba ya maji wanaswa

T L