Habari

Makanisa yatumia teknolojia kusajili waumini kwa ibada

July 19th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MAKANISA yamelazimika kutumia teknolojia kusajili waumini kuhudhuria ibada kufuatia kanuni mpya za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Baadhi ya makanisa yamebuni programu za mitandao ambazo waumini wanatumia kujisajili watengewe viti kanisani.

Hii inasaidia kuhakikisha wamechagua watu 100 wanaopaswa kuhudhuria kila ibada kwa wakati mmoja.

Katika mwongozo wa kufungua maeneo ya ibada, baraza la viongozi wa kidini liliagiza watu wasizidi 100 katika kila ibada na waketi umbali wa mita moja na nusu kutoka kila mmoja.

Kulingana na wasimamizi wa Kanisa la Deliverance mtaani Waithaka, waumini wanatakiwa kujisajili katika programu maalumu ya kanisa hilo ili watengewe vita kanisani.

“Hii inahakikisha hakuna msongamano watu waking’ang’ania nafasi 100 wahudhurie ibada. Kila anayejisajili anatengewa nafasi ya kuketi katika mojawapo ya ibada,” amesema pasta Amos Warui wa kanisa hilo.

Programu hiyo ilibuniwa na kamati ya kudhibiti corona ya kanisa hilo.

Baraza la viongozi wa kidini, iliagiza kila eneo la ibada kuunda kamati ya kuhakikisha mwongozo wa kufungua makanisa na misikiti unafuatwa.

Makanisa mengi yanatumia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kupanga ibada.

Yaliwataka waumini kujisajili wapange idadi ya ibada ikizingatiwa kuwa kila moja inapaswa kuchukua muda wa saa moja.

“Kwa sababu watu wengi wanatumia mtandao wa WhatsApp, tuliutumia kufahamisha waumini mikakati yetu ya kufungua kanisa. Kwa sababu tumekuwa tukiutumia mwa muda kuwasiliana na waumini, tuliweza kupanga ibada zetu kwa urahisi kwa kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya,” akasema mwenyekiti wa kamati ya kanisa Katoliki mjini Machakos Dominic Kaleli.

Makanisa yaliyo na chini ya waumini 100 hayakutatizika kupanga ibada japo yalizingatia kanuni za wizara ya afya.

Viongozi wa kamati za kuzuia msambao wa corona katika makanisa mengj kaunti ya Machakos hayakuruhusu watu kukusanyika baada ya ibada ilivyokuwa ikifanyika kabla ya corona kuripotiwa nchini.

Serikali ilipofunga makanisa, mengi yalianza kutoa ibada kupitia mitandao.

Baada ya baraza la viongozi wa kidini kutangaza kufunguliwa kwa maeneo ya ibada, baadhi ya makanisa yalisema hayatafungua.