Habari Mseto

Makao makuu ya Coca-cola Kenya kuuzwa

June 18th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Jumba la kibiashara linalomilikiwa na kampuni ya kutengeneza soda ya Coca-Cola sasa linauzwa.

Jumba hilo la orofa tatu na lililojengwa kwenye ekari 3.26 limo eneo laUpper Hill, Nairobi na lilitangazwa na kampuni ya Knight Frank kuwa limo sokoni.

Kampuni hiyo ilituma ujumbe kwa watu au mashirika yanayoazimia kununua jumba hilo kutuma ombi la kuonyesha azimio lao kabla au Julai 4.

Jumba hilo lina nafasi 130 za maegesho pamoja na ukumbi wa mikutano, chumba cha mazoezi, na mkahawa.

Kulingana na notisi hiyo, jumba hilo linafaa zaidi kuwa makao makuu ya afisi za chuo kikuu.

Jumba hilo lilikuwa ni makao makuu ya eneo la Afrika Mashariki, Kati na Afrika Magharibi na yalikuwa yakihudumia mataifa 14 barani Afrika.

Kampuni hiyo ilihamishia makao hayo katika jumba jipya la 90 James Gichuru. Meneja wake wa eneo Ahmed Rady alisema hatua ya kuhama itaisaidia kampuni hiyo katika operesheni zake, katika eneo wazi na ambalo sio rasmi sana, karibu na maeneo ya makazi kwa lengo la kuwapa motisha wafanyikazi wake.

Coca-cola, iliyo na makao yake makuu Atlanta Georgia ni moja kati ya kampuni tajiri zaidi ulimwenguni.

Lakini Knight Frank haikutoa habari kuhusiana na kiwango cha fedha inachouza jumba hilo ila eneo la Upper Hill huuzwa kwa kati ya Sh500 milioni na Sh600 milioni kwa ekari moja.