Habari Mseto

Makarani kuwasilisha mswada bungeni kulinda maslahi yao

April 12th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Makarani wa ofisini wanaunda mswada wa kuwasilisha mbele ya bunge la kitaifa ambao utasaidia kuinua viwango na maslahi ya kazi zao na kutambua muungano wao kisheria.

Katika mswada huo, makarani hao aidha wananuia kuunda chuo cha mafunzo ya kitaaluma ya ukatibu ili kunoa taaluma yao kutoa wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu.

Haya yalisemwa Alhamisi wakati zaidi ya makarani 2,000 kutoka kote nchini walipokutana katika hoteli ya Kunste, mjini Nakuru kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mambo muhimu ambayo mswada huo unafaa kujumuisha.

Kulingana na viongozi wa muungano wao wa Kenya National Secretaries Association (KENASA), endapo bunge la taifa litapitisha mswada huo, makatibu kote nchini wataweza kupata mazingira bora ya kazi, elimu ya juu na kupata ujuzi wa kikazi.

“Nia kuu ya mswada huu ni kunyoosha namna kazi ya makatibu inavyofanywa na kufanya taaluma yetu iwiane na taaluma nyingine kuu,” akasema mwenyekiti wa KENASA, Bw Andrew Osundwa.

Makarani hao waliungana na wajumbe kutoka Tanzania, Uganda na Marekani kusherehekea siku ya kusherehekea Uhuru wa Makarani Duniani.

Kulingana nao, Kenya ina zaidi ya makarani  5,500 huku kukiwa na walioongeza elimu kufikia viwango vya shahada za uzamifu, uzamili na shahada.

Aidha, chuo ambacho wanataaluma hao wanauia kujenga kitasaidia kutoa mafunzo ya kitaaluma kwa makatibu na kusaidia kukagua ubora wa mafunzo yanayotolewa ya taaluma hiyo.

“Wakati mwingine taaluma hii hudharauliwa lakini sasa tumeweza kuongeza elimu na kuboresha namna tunavyofanya kazi,” Bw Osundwa akasema.

Katibu msimamizi wa maslahi ya wafanyakazi katika wizara ya huduma za umma Bw Simon Angote aliyehudhuria hafla hiyo alisema serikali imefanya juhudi ili kuinua viwango vya taaluma hiyo, akisema sasa kuna vyuo vinavyotoa masomo ya juu.

“Mtu wa muhimu katika kazi ya kuelezea kuhusu afisi hata za maafisa wakuu serikalini na kuhusu namna ilivyopangwa ni katibu na hivyo serikali imejifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa taaluma hii inaimarishwa,” akasema Bw Angote.