Michezo

MAKARIOS: Timu inayokuza vipaji vya soka mtaani Riruta

May 22nd, 2018 2 min read

Na PATRICK KILAVUKA

RIRUTA United (Makarios) ni timu ambayo inapatikana mtaa wa Riruta uwanja wao wa kuchezea ukiwa Kinyanjui Technical, Nairobi. 

Ilistawishwa mwishoni mwa mwaka 2017 baada ya muafaka kuafikiwa na wachezaji wa eneo la Riruta ambao walikuwa wanasakatia timu mbalimbali za eneo hilo kuhisi kwamba, litakuwa jambo njema kuziwianisha timu za mtaani kujenga himaya kubwa ya soka kulea vipawa kwa minajili ya kucheza soka ya hadhi nchini au ughaibuni.

Baada ya wazo hilo kupokelewa kwa moyo mkunjufu, wadau wa timu waliiuzia jamii kubwa ya Riruta sera hiyo na ikapata mashiko na timu ikaundwa na  inanawiri.

Riruta United ikufanya mazoezi. Picha/ Patrick Kilavuka

“Tulielezea wanasoka mbalimbali kuhusu nia ya kujenga timu moja nzito ambayo inaweza kuwa kitovu cha soka kwa timu za mtaani ili turahisishe uwajibikaji, kuimarisha uwezo wa kuishughulikia na hoja yetu ikaitikiwa,” aeleza kinara wa timu Geofrey  Sirima ambaye alikuwa mchezaji wa timu ya Amani Yasset.

Anashirikiana sako kwa bako na meneja wa timu Geofrey Kilei ( aliyeichezea Amani Yasset), kocha George Wafula ( mchezaji wa zamani wa Kibera Olympic), naibu wake Geofrey Osoro (Yasset na Makarios), Katibu mkuu Josphat Karuri  aliye Mwekahazina wa FKF, Tawi la Nairobi Magharibi na kapteni Ford Ikutwa.

Hata hivyo, wachezaji wengi wa timu hii walitoka katika vilabu mashuhuri mtaani humo kama Riruta na Amani Yasset lakini milango ilifunguliwa kwa wachezaji ambao wako radhi kusajiliwa kama njia ya kuleta umoja na nguvu katika kujenga Jamii ya soka ambayo itakuwa nembo ya mtaa.

“Asilimia kubwa ilitoka kwa timu zilizotajwa japo wengine wamesajiliwa kutoka  timu zingine za mtaa ili kuanza kuipa sura ya mtaa na umaarufu unaohitajika kutesa katika ulimwengu wa soka katika patashika la ligi ya FKF, Primia na kucheza barani majaliwa,” adokeza kinara Sirima.

Meneja wa timu Geofrey Kilei akiwanoa vijana wake jinsi ya kuzima wapinzani. Picha/ Patrick Kilavuka

Kulingana na mwenyekiti huyo, matunda yalianza kuonekana kupitia michezo yao ya kujipima nguvu na za ligi ya FKF, Tawi la Nairobi Magharibi.

“Hii ilikuwa baada ya kucheza katika kombe la Dagoretti na kuwahi robo fainali baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Olympic Talented. Ingawa hivyo, timu hiyo pinzani ilikuwa na kikosi cha wachezaji mahiri ambao wanapiga soka ya hadhi kama Jesse Were miongoni mwa wengine,” asema Sirima na kuongezea kuwa walicheza tena dimba la kombe Chris Darling na kubanduliwa katika mkumbo wa pili.

Baada ya kujisuka huko, timu hii ilijitwika jukumu nzito la kujisajili kwenye ligi ya Kanda, Tawi la Nairobi Magharibi baada ya kuhifadhi nafasi ya Makarios. Sasa wanasukuma gurudumu la soka katika daraja hiyo wakiwa na matumaini ya kufanya vyema.

Kufikia kuandikwa kwa makala haya, walikuwa wamesakata mechi saba za ligi hiyo na kuzoa pointi 12.

Makarios wakijiandaa kwa mechi. Picha/ Patrick Kilavuka

Michuano ambayo wameibuka washindi ni dhidi ya South B Allstars ambapo waliipachika 1-0, kutandika Nairobi Prisons 2-1, kuwabwaga mabingwa wa kombe la Chapa Dimba Kaunti ya Nairobi AFC Leopards Youth 2-1, kuigonga Kitisuru Allstars 2-1 kabla kupoteza mechi zake dhidi ya Gogo Boys 1-0, Slum Dwellers 2-0 na ile ya South B Sportive ambapo waliwanyamazishwa 3-2.

Mpango? Kuwatolea ushauri wa kiroho kupitia wachungaji, kusaidiana kwa hali na mali kwani wachezaji ni wale hawana kazi maalum na wanatoka katika jamii zenye uwezo wa chini, kutembeleana kama njia ya kujifahamisha na jamii zao na kujuana zaidi, kutafuta wafadhili na kukumbatia walioko kama Makarios, Orthodox, Radio mtaani na wafanyabiashara kuisaidia timu.

Kando na hayo kuhimizana kuwajibika, kuwasajili wachezaji na kuwaangazia katika majukwaa ya kitaifa na ughaibuni, timu kuwa kama familia moja na kujaribu kuwaleta pamoja wachezaji wa zamani ili waisaidie kukuza vipaji vya kandanda mtaani, kutiana moyo na kutumainiana moja kwa mwingine maishani wakikuza talanta zao kwani nani ajuaye ya kesho!