Habari Mseto

Makasisi wa ACK waliofutwa kulipwa Sh6.8 milioni

December 21st, 2018 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

MAKASISI wa kanisa la ACK Kaunti ya Nyeri ambao walikuwa wametimuliwa kutoka kazi zao za upasta kuhusiana na madai ya ushoga hatimaye wamelipwa Sh6.8milioni kutoka kwa kanisa hilo, baada ya vita vya miaka minne mahakamani.

Korti iliamua kuwa kanisa hilo liwalipe pesa hizo, kugharamia matatizo ya kisaikolojia ambayo walipitia wakati walisimamishwa kazi zao za uhubiri.

Malipo hayo aidha yanahusisha mshahara ambao hawakulipwa, pamoja na manufaa mengine waliyokosa kufuatia hatua ya leseni zao za kikazi kutwaliwa na kanisa.

Walisimamishwa kazi mnamo Agosti 2015, lakini Septemba 2016 korti ikaamuru warejeshwe kazini baada ya kubaini kuwa kutimuliwa kwao kulikiuka sheria.

Bw John Gachau atapokea Sh2.4milioni, huku James Maigua na Paul Warui wakipokea Sh2.2milioni kila mmoja.

Jaji Nzioki Wa Makau wa mahakama ya kutatua mizozo baina ya waajiri na wafanyakazi Jumatano aliruhusu maombi ya wahubiri hao kuwa pesa hizo ziachiliwe ziwafikie.

Askofu wa eneo la Mlima Kenya Magharibi Joseph Mwangi Kagunda alikuwa amepinga ombi hilo, akiitaka korti kutoachilia pesa hizo.

Bw Kagunda alieleza korti kuwa uamuzi wa Septemba 2016 ulikuwa na makossa. Alisema kuwa mali ya kanisa hilo katika maeneo tofauti nchini husimamiwa na makamishna wa makanisa Kenya, ilhali walizuiwa na mahakama kujiunga na kesi hiyo.

“Kufuatia hatua ya makamishna hao kuzuiwa na korti kujiunga na kesi hii, sasa hawawezi kuadhibiwa na maamuzi kutoka kwa kesi,” akasema askofu huyo kupitia wakili wake.

Lakini wahubiri wao kupitia wakili David Onsare walipinga wakisema kuwa muda wote huo, kanisa lilikosa kufuata amri za korti.

Mnamo Mei, korti ilipiga kanisa hilo faini ya Sh200,000 kwa kukosa kuwarejesha wahubiri hao kazini.

Bishop Kagunda aidha mnamo Julai 12 alihukumiwa na korti kwa kuidharau.