Habari Mseto

Makasisi waliotimuliwa kuhusu ushoga wataka korti iadhibu kanisa

March 6th, 2018 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

KANISA Anglikana la Kenya limepuuzilia mbali ombi lililowasilishwa mahakamani na makasisi watatu ambao wanataka ibainishwe lilikiuka agizo la mahakama.

Watatu hao walikuwa wamesimamishwa kazi baada ya kuhusishwa na vitendo vya ushoga.

Kupitia kwa wakili William Muthe, Wadhamini Waliosajiliwa wa Kanisa Anglikana walisema ombi la makasisi hao katika Mahakama ya Leba ya Nyeri halifai.

Makasisi hao John Gachau, James Maigua na Paul Warui, walikuwa wamewasilisha ombi hilo kutaka wadhamini hao waadhibiwe kwa kukiuka agizo lililoamrisha warudishwe kazini.

idha, kupitia kwa wakili wao, Bw Donald Onsare, walimwomba Jaji Nzioki wa Makau aagize wadhamini hao wafungwe gerezani kwa miezi sita kwa kukosa kuwalipa ridhaa ya Sh6.8 milioni.

Walisema wadhamini wa kanisa hilo wamepuuza maagizo mawili yaliyotolewa na Mahakama ya Leba mnamo Septemba 30, 2016.

“Hatua ya washtakiwa kupuuza na kutotii agizo la mahakama ni dharau kwa mahakama hii ya heshima na ni lazima tabia hiyo iadhibiwe,” akasema Bw Onsare.

Alisema kanisa halijatii maagizo hayo licha ya kuwa yaliwasilishwa, na akatoa wito hatua ichukuliwe ili kulinda hadhi na mamlaka ya mahakama.

Wakili huyo alieleza kuwa msimamo wa kanisa kutotii agizo la mahakama unaathiri makasisi hao vibaya na hivyo basi kuwazidishia matatizo ya kimawazo.

Wakijitetea, wadhamini hao walisema ombi hilo lina dosari kubwa na halina msingi kisheria.

Wakili Muthee alisema afisi ya wadhamini wa kanisa ni shirika lililosajiliwa na hivyo basi haiwezekani kulihukumu kifungo cha gerezani.

“Ombi hili halijatimiza matakwa ya Sheria za Ukiukaji wa Maagizo ya Mahakama. Jinsi lilivyonakiliwa, haliwezi kukubalika,” akasema Bw Muthee.

 

 

 

 

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Aprili 5, 2018 mbele ya Jaji Nzioki Makau katika Mahakama ya Leba ya Nyeri.