MAKAVAZI CUP: Omariba, Sakawa waibuka mabingwa wa vishale

MAKAVAZI CUP: Omariba, Sakawa waibuka mabingwa wa vishale

Na JOHN KIMWERE

WARUSHA vishale Wycliffe ‘Onetouch’ Omariba na Selina Sakawa wote wa Museum Darts wameibuka mabingwa wa shindano la Makavazi Cup kwa wanaume na wanawake mtawalia.

Kwenye ngarambe hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Gerish Hotel, Mitheru Kaunti ya Tharaka Nithi, Omariba alishinda Peter Wanjie wa Admistration Police kwa seti 5-4 katika fainali.

Katika fainali ya wanawake, Sakawa alimfinya Ann Macharia wa Kenya Prisons (Magereza) kwa seti 5-3.

”Ninashukuru Mungu kwa ushindi wakati ambapo tumeanza kurejea kwa hali ya kawaida baada ya janga la corona kuvuruga shughuli za spoti nchini,” Sakawa alisema na kuongeza kuwa anatarajia kuendelea hivyo kwenye mashindano ya mwisho mwaka huu 2021.

Selina Sakawa akituzwa baada ya kuibuka bingwa kitengo cha wanawake. PICHA | JOHN KIMWERE

Pia Omariba anasema kuwa amejaa furaha tele kufuatia ufanisi huo maana wapinzani wote hawakuwa rahisi.

Kitengo cha wanaume, Wanjie aliibuka mfungaji bora alipopiga alama 180 mara nne naye Munene alituzwa kwa kuibuka bora alipozoa pointi 161 akutumia mshale mmoja akimalizia mchezo wake.

Naye Sakawa alitwaa tuzo ya mchezaji bora alisajili alama 180 mara mbili kwa wanawake.

Kwenye nusu fainali, Omariba alinyuka David Gaitho wa Stima Club seti 4-0 naye Peter Wanjie alisajili ushindi wa seti 4-0 dhidi ya Charles Munene.

Kwa wanawake, Sakawa alibeba ufanisi wa seti 4-2 dhidi ya Leah Chumba huku Regina Nyaga akishindwa na Ann kwa seti 4-3.

Gaitho na Chumba walimaliza nafasi ya tatu kwa kuzoa seti 4-2 na 3-1 dhidi ya Munene na Nyaga kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia.

Mashindano hayo yalivutia zaidi ya wachezaji 100 kutoka kaunti nchini ikiwamo Tharaka, Embu na Nairobi.

You can share this post!

Kenya kusaka leo tiketi ya Kombe la Dunia la walemavu

Wanaotaka kumrithi Uhuru wafuatilia hotuba yake bungeni

T L