Makomando wawinda Kangogo

Makomando wawinda Kangogo

Na WAANDISHI WETU

MAKACHERO wanaochunguza afisa wa polisi wa cheo cha Koplo Caroline Jemutai Kangogo, anayesakwa kuhusiana na visa vya mauaji, wamebaini kwamba alikuwa akishiriki sakata kadhaa na polisi wenzake ambao wanaendelea kuficha maelezo yanayoweza kusaidia kukamatwa kwake.

Taifa Leo Jumatatu ilipata habari muhimu zilizofichua kuwa, kuna makundi mawili ya maafisa wa polisi wanaoshiriki vitendo vya uhalifu, katika Bonde la Ufa, na Bi Kangogo alikuwa sehemu ya moja wa makundi hayo.

Kulingana na vidokezo vya afisa wa polisi ambaye hakutaka watajwe, Bi Kangogo na maafisa hao walikuwa wakishiriki visa vya wizi wa kimabavu, uporaji wakishirikiana na wanasiasa na wafanyabiashara matajiri katika maeneo ya Nakuru, Eldoret, Kapsabet na Kericho kati ya miji mingine ya Bonde la Ufa.

Afisa mmoja anayehusika na uchunguzi huo alisema kuna utata mwingi na masuala yasiyofahamika na umma kuhusu mauaji ya John Ogweno na Peter Ndwiga Jumatatu ilyopita.

Bi Kangogo ndiye alitekeleza mauaji ya wawili hao kwa kuwapiga risasi.

Bw Ogweno ambaye alikuwa afisa wa polisi wa cheo cha konstebo alipatikana ameuawa ndani ya gari lake katika kituo cha polisi cha Kasarani, Nakuru huku mwili wa Bw Ndwiga pia ukipatikana ndani ya chumba cha hoteli katika Kaunti ya Kiambu.

Afisa wa cheo cha sajini Joseph Ologe alipata mwili wa Bw Ogweno ukiwa na majeraha mengi ya risasi ndani ya gari lake aina ya Toyota Corolla yenye nambari ya usajili KBV 735 katika kituo hicho cha Kasarani.

“Kuna kundi la polisi ambao wanataka wamuue huku kundi jingine likiapa kumlinda ndiyo maana hajaonekana,” akasema afisa huyo.

Huku Bi Kangogo ambaye bado anasakwa akilaumiwa kwa mauaji ya Bw Ogweno, Taifa Leo imebaini zaidi ya watu wanne wanachunguzwa kutokana na mauaji ya Bw Ndwiga ambaye alikuwa afisa wa zamani wa polisi na alimiliki kampuni inayotoa huduma za usalama yenye makao yake Juja.

Afisa wa DCI Katika Kaunti ya Nakuru Anthony Sunguti alisema, huenda marehemu Ogweno aliuawa na zaidi ya mtu mmoja. Mauaji hayo huenda yalitekelezwa na watu wa ndani ya idara hiyo na huenda polisi walihusika na mauaji hayo.

Vidokezo vingine kutoka DCI eneo la Juja ni kuwa madai ya Mabw Ndwiga na Ogweno kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bi Kangogo yalikuwa uongo na yanatumiwa tu kufunika mauaji hayo.

“Kile ambacho kinafaa kifanyike sasa ni Bi Kangogo kupewa ulinzi mkali kwa kuwa kuna maafisa wa ngazi za juu katika idara ya polisi wanaotaka kumuua. Akamatwe na apewe nafasi ya kusimulia kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu,” akasema afisa huyo.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: HIV: Maelfu wakwepa tembe za PrEP,...

Matamanio ya Ruto, uamuzi wa June na mja kupata ajaliwalo...