Habari Mseto

MAKOVO MBATHA: Wengi hawakutarajia ningefika hapa

April 29th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

AKIWA mdogo alitamani kuwa polisi, padri ama mwanajeshi kama ilivyo kwa wengi wao miongoni mwa jamii yao katika Kaunti ya Makueni. Hata hivyo leo hii wengi wao hawaamini jinsi alivyoibuka kati ya wasanii wanaofanya mengi katika sekta ya uigizaji.

Makovo Mbatha ni msanii anayejivunia kuigiza filamu nyingi tu na kupata mpenyo kuonyeshwa kupitia runinga tofauti hapa nchini. Pia anajivunia kuwa mwelekezi wa filamu taaluma aliyoanza mwaka 2012.

Aidha ameodhoreshwa kati ya wasanii wanaomiliki brandi za kuzalisha filamu nchini ambapo tayari ametoa nafasi za ajira kwa waigizaji wengine 12 wanaume na wanawake.

Alianzisha brandi iitwayo Do Arts Centre mwaka 2016 ili kusaidia waigizaji wanaokuja ambapo huzalisha filamu wakitumia mwongozo wa vitabu za riwaya (setbooks). Kadhalika huandaa na kutayarisha kipindi kiitwacho Kilimo ambapo hupeperushwa kupitia runinga ya KBC kila Jumapili tangu mwaka 2015.

Kabla ya kuanzisha brandi hiyo alifanikiwa kufanya na makundi kadhaa ikiwamo Jawabu Productions, Milestone Stalling na Fanaka Arts.

Makovo Mbatha alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali. Picha/ John Kimwere

Kadhalika alishiriki uigizaji wa sauti katika matangazo ya kibiashara na kampuni kadhaa hapa nchini.

”Hakika nimefanya mengi kinyume na yaliyokuwa matarajio ya wengi hasa katika familia yangu ambapo mwanzo baadhi yao waliokuwa wakinipiga kujiunga na uigizaji,” alisema na kuongeza kuwa alivutiwa na masuala ya uigizaji mwaka 2017 akiwa kidato cha tatu alipotuzwa kwa kuibuka msimulizi mwema katika Mkoa wa Mashariki.

Msanii huyu anasema kuwa mwaka 2015 alishiriki filamu kama ‘Faith’ ‘Act of Charity,’ na ‘Good Deeds’ zilizopata mpenyo kurushwa kupitia Ebru TV. Vile vile aliwahi kuigiza filamu za TV Series ikiwamo ‘Kijakazi,’ ‘Sumu la Penzi,’ zilizopeperushwa kupitia Maisha Magic East pia ‘Radhi’ ilionyeshwa kupitia Foxlife TV.

Mapema mwezi huu alikuwa miongoni mwa wasanii waliohusika kwenye juhudi za kuzalisha filamu kwa jina ‘The Lady in Red’ iliyotengenezwa na kundi liitwalo Son of Man International.

”Pia ninalenga kupata nafasi kuandaa kipindi kwenye mojawapo kati ya redio za humu nchini siku sijazo,” alisema na kuongeza kuwa anaamini muda utakapowadia hakutakuwa na wa kumtia breki. Picha/ John Kimwere

”Katika mpango mzima nimezamia kwenye uigizaji wa sauti nataka kuibuka kati ya waigizaji mahiri duniani,” alisema na kuongeza kwamba katika taaluma hiyo huwa vigumu watu kufahamu sauti yako maana hakuna mahali unapoonekana sura.

Katika matangazo ya kibiashara amefanya na kampuni kadhaa ikiwamo Safaricom-Shangwe, Safaricom-Mtaani aliposhiriki kwa uigizaji wa sauti, bila kuweka katika kaburi la sahau KTN- Breaking News.

Anasema anatamani sana kuzalisha filamu bora za hadhi ya Hollywood pia kufanya kazi na wana maigizo wa Afrika Kusini maana sekta hiyo inaendelea kufanya vizuri katika taifa hilo.