Makuhani wa usaliti

Makuhani wa usaliti

Na WANDERI KAMAU

MVUTANO na majibizano ya kisiasa yanayoshuhudiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto ni matokeo ya usaliti kwenye mikataba ya awali ya kisiasa kati ya vigogo wakuu wa kisiasa nchini.

Tangu handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga mnamo Machi 2018, uhusiano kati ya Rais na naibu wake ulianza kudorora.

Uhusiano huo umekuwa mbaya kiasi kwamba, wawili hao sasa wameanza kurushiana maneno bila kuogopa, kinyume na ilivyokuwa awali mwanzoni mwa utawala wao.

Mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta alimwambia Dkt Ruto kujiuzulu serikalini, badala ya kuendelea kuikosoa kwa upande mmoja, huku akiisifu kwa upande mwingine kutokana na miradi iliyofanya.

“Kwa upande mmoja, unasema serikali imefeli. Kwa upande mwingine, unasema maendeleo ambayo imefanya. Huo ni unafiki. Huwezi kuwa unarejelea yale serikali unayohudumu imekosa kufanya wakati ukitaja mafanikio yake. Ni heri ujiuzulu!” akafoka Rais Kenyatta kwenye ujumbe aliomwelekeza naibu wake moja kwa moja.

Mnamo Jumamosi, Dkt Ruto alimjibu Rais kwa kusema ataendelea kuhudumu kwenye serikali, akisema walishiriki kutafuta kura pamoja.

“Nitaendelea kuhudumu kama Naibu Rais kwani hiyo ndiyo nafasi yangu kikatiba,” akasema Dkt Ruto alipohutubu katika Kaunti ya Isiolo.

Wadadisi wanataja kuvurugika Chama cha Jubilee (JP) na mkataba kati ya wawili hao kama hali ya kawaida ambayo imekuwepo kwa muda mrefu katika ulingo wa siasa nchini.

Mnamo 2018, hatua ya Bw Odinga kubuni handisheki ilikuwa mwanzo wa mwisho wa muungano wa National Super Alliance (NASA) uliomshirikisha Bw Odinga, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), Bw Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

Watatu hao walimuunga mkono Bw Odinga kuwania urais mnamo 2017.

Hata hivyo, walidai “kusalitiwa” na Bw Odinga kupitia handisheki, wakisema hakuwaambia alipoanza kushauriana na Rais Kenyatta.

Bw Musyoka pia alidai “kusalitiwa” na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, kwa kukosa kumuunga kuwania urais 2013.

Kulingana na Bw Musyoka, Rais Kibaki alikuwa amemwahidi kumuunga mkono, hasa kutokana na mchango wake wa kuongoza harakati za kuyashinikiza mataifa mbalimbali kuunga mkono wito wa Kenya kwayo kujiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Bw Musyoka alisema ahadi hiyo pia ilitokana na tashwishi ilyokuwepo kuhusu ikiwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto wangewania urais kutokana na mashtaka yaliyowakabili katika mahakama hiyo kutokana na uchaguzi tata wa 2007.

“Sijui hali ilivyobadilika hadi sasa,” akasema Bw Musyoka, aliyehudumu kama makamu wa rais katika Serikali ya Muungano kati ya 2008 na 2013.

‘Usaliti’ mwingine unadaiwa kufanywa dhidi ya Bw Mudavadi na Rais Kenyatta na Dkt Ruto mnamo 2012, ikielezwa walimwahidi kumuunga mkono kuwania urais 2013.

Sawa na yaliyomkumba Kalonzo, sababu kuu ilitokana na tashwishi iliyokuwepo kuhusu ikiwa wawili hao wangewania urais kutokana na mashtaka ya ICC.

Hadi sasa, Bw Mudavadi anashikilia kuwa ndiye aliyepaswa kuungwa mkono na wawili hao kwani walikuwa tayari washabuni mwafaka wa kisiasa, lakini “wakamruka.” Rais Kenyatta alinukuliwa akisema alizubaishwa na ‘madimoni’ (mashetani) kutia saini mkataba wa kisiasa na Bw Mudavadi.

Wadadisi wanataja matukio hayo kuwa ishara tosha kuwa lengo kuu la wanasiasa nchini huwa ni jinsi watakavyojifaidi wao wenyewe kwenye mikataba wanayobuni.

Mdadisi wa siasa Javas Bigambo anasema mwelekeo huo unajenga mazingira ambapo ni vigumu hali ya kuaminiana kuwepo katika ulingo wa siasa nchini.

“Ikiwa wanasiasa wanaweza kusalitiana baina yao, je, ni kiasi kipi wanaweza kuwasaliti wananchi waliowachagua ili kuwahudumia? Hii ni hali inayopaswa kuchukuliwa kwa uzito,” akasema jana kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kwa upande wake, Prof Macharia Munene anasema kuwa msingi mkuu wa ushirikiano wowote wa kisiasa ni maslahi ya pande husika.

Anataja hili kuwepo hata katika nchi zilizostawi kidemokrasia kama Amerika na Uingereza.

“Hali ya mikataba kubuniwa na kuvunjika ni jambo la kawaida katika siasa, kwani lengo kuu la wahusika huwa ni kuona ikiwa watatimiza maslahi yao,” akasema.

Hata hivyo, anasema kilicho muhimu ni uwepo wa taasisi muhimu kama vyama, ili kuhakikisha vinajisimamia kwa njia huru hata baada ya viongozi wakuu kuondoka.

You can share this post!

Wanaharakati waitaka serikali kupiga marufuku matumizi yote...

Askofu aonya wanaume dhidi ya kutumia ‘viagra’...