Kimataifa

Makundi ya kutetea haki yataka Bashir apelekwe Hague haraka

February 13th, 2020 2 min read

Na AFP

KHARTOUM, Sudan

MAKUNDI ya kutetea haki nchini Sudan yameitaka serikali ya mpito inayoongowa na baraza la majeshi na wale wa kiraia limwasilishe aliyekuwa kiongozi wa nchini hiyo Omar al-Bashir kwa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).

Yanataka Rais huyo aliyeondolewa uongozini Aprili 2019 afunguliwe mashtaka kwa kuhusika na mauaji ya halaiki yaliyotekelezwa katika jimbo la Darfur mnamo mwaka wa 2003.

Mnamo Jumanne watawala wapya wa Sudan walikubaliana na viongozi wa makundi ya waasi walikubali kumpeleka Bashir, na wasaidizi wake watatu wa zamani, katika mahakama hiyo iliyoko jijini The Hague, Uholanzi ili wajibu mashtaka kuhusiana na mauaji ya halaiki Darfur.

“Watawala wa Sudana wanapasa kubadilisha maneno yao kuwa vitendo mara moja na wawasilishe al-Bashir na wengine katika mahakama ya ICCI jijini The Hague,” kaimu katibu mkuu wa shirika la kutetea haki, Amnesty International Julie Verhaar akasema.

“Omar al-Bashir anasakwa na mahakama ya ICC kuhusu mauaji, matesa na ubakaji wa maelefu ya watu wakati wa mapigano ya Darfur. Na uamuzi wa kumwasilisha kwa mahakama hiyo ni hatua nzuri katika juhudi za kupata haki kwa waathiri na familia zao,” afisa huyo akaongeza.

Mapigano katika eneo la Darfur yalitokea wakati kundi la wapiganaji wa kikabila walipopigana wanajeshi wa serikali ya Bashir walilalamikia kutengwa kisiasa na kiuchumi.

Mahakama ya ICC inamtuhumu Bashir kwa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya kibinadamu yaliyotekeleza dhidi ya raia na wanajeshi wa serikali yake wakishirikiana na wapiganaji wa Janjaweed.

Lakini Bashir, ambaye wakati huu amefungwa gerezani nchini Sudan baada ya kushtakiwa kwa ufisadi, amekana madai hayo na amekwepa kukamatwa kwa zaidi ya miaka 10.

ICC pia iliwatuhumu Ahmed Haroon, Abdulrahim Mohamed Hussain na Ali Kushied ambao walikuwa wandani wa al Bashir.

Mnamo Jumanne Mohamed Hassan Al –Taishay ambaye ni mwanachama wa Baraza la kijeshi alisema, “ Bashir na wengine watatu wanaotakiwa na ICC sharti waende huko”.

“Tumekubaliana kwamba tutaunga mkono ICC na kwamba wahalifu hao wanne watawasilishwa huko,” Taishay akasema kwenye kikao na wanahabari katika jiji la Juba, nchini Sudan Kusini.

Ujumbe wa Serikali umekuwa ukikutana na viongozi wa makundi ya waasi kutoka eneo la Darfur jijini humo. Hata hivyo, Taishay hakusema ni lini washukiwa hao wanne watawasilishwa jijini The Hague.