Michezo

Makwata afunga Zesco ikilimwa Zambia

February 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Ian Otieno (kipa), David Owino (beki) na John Makwata (mshambuliaji) walikuwa na siku mbaya kwenye Ligi Kuu ya soka ya Zambia baada ya timu yao ya Zesco United kupoteza 2-1 dhidi ya NAPSA Stars, Jumapili.

Mabingwa watetezi Zesco, ambao pia wameajiri mvamizi Jesse Were kutoka Kenya ambaye hakushiriki mchuano huo, walizamishwa na magoli kutoka kwa Aaron Kabwe na Colins Sikombe yaliyopatikana dakika ya 40 na 52, mtawalia.

Makwata alifungia waajiri hao wake wapya bao la kufutia machozi dakika ya 89.

Tangu ajiunge na Zesco mnamo Januari 31 kutoka AFC Leopards aliyokuwa amefungia mabao 13, Makwata amechangia mabao matatu katika mechi tatu ligini dhidi ya Mufulira Wanderers (Februari 9), Power Dynamos (Februari 16) na NAPSA Stars (Februari 23).

Nkana, ambayo imeajiri beki Mkenya Musa Mohamed, iliridhika na alama moja katika sare tasa dhidi ya Kansanshi.

Forest Rangers inaongoza kwa alama 43 ikifuatiwa na Green Eagles (41), Nkana (40), Zesco (39) nayo NAPSA Stars inafunga mduata wa tano-bora (39).