Michezo

Makwata apata hat-trick ZESCO ikinyonga Neelkhant

September 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA John Makwata na Jesse Were waliona lango na kusaidia timu yao ya ZESCO United kuponda Neelkhant Lime 8-0 Septemba 21 katika mechi ya kujiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zambia.

Mshambuliaji wa zamani wa AFC Leopards na Ulinzi Stars, Makwata alitikisa nyavu za Neelkhant, ambayo imeingia Ligi ya Daraja ya Pili, mara tatu, huku mvamizi matata Were akichangia goli moja.

Mabao zaidi yalipatikana kupitia kwa Kelvin Kampamba (mawili), Bruce Musakanya na Logic Ching’andu.

Mbali na Were na Makwata ambao waliibuka wafungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Kenya mwaka 2015 na 2016 mtawalia, Zesco pia imeajiri Wakenya David Owino (beki) na Ian Otieno (kipa).

Zesco haitashiriki mashindano yoyote ya Bara Afrika msimu 2021-2020 kwa hivyo itaeleza nguvu zake zote kwenye mashindano ya nchini Zambia. Wanaumeme hao walipoteza ubingwa wa ligi kwa Forest Rangers, huku wanabenki wa Zanaco wakifuzu kushiriki Kombe la Mashirikisho.

Ligi Kuu ya Zambia imeshuhudia wachezaji wa Kenya wakimiminika humo miaka ya hivi karibuni. Haron Shakava, Duncan Otieno, Duke Abuya (Nkana) na Timothy Otieno na Shaaban Odhoji (Napsa Stars) pia wako katika orodha ya Wakenya waonogesha ligi hiyo.