Habari Mseto

Malala akana kudaiwa Sh8 milioni na KRA

August 14th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kaunti ya Kakamega Cleophas Malala amesema madai kuwa akaunti zake za benki zitafungwa ni sehemu ya mipango ya kumtisha ili abadili msimamo wake kuhusu mfumo tata wa ugavi wa fedha baina ya kaunti.

Bw Malala Ijumaa alifafanua kuwa ametoa ushahidi kwa maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) kuwa ametimiza masharti yote ya ulipaji ushuru.

“Nimefanya kikao na Naibu Kamishna wa idara ya ushuru wa ndani Daniel Kagira ambaye amenihakikishia kuwa hali yangu ya ulipaji ushuru ni shwari,” akasema Bw Malala.

Akaongeza: “Imethibitishwa katika akaunti zangu zoye kwa sidaiwi na KRA pesa zozote bali ninaidai asasi hiyo Sh324.”

Seneta Malala alishutumu kiranja wa wengi Irung’u Kang’ata kwa kujaribu kumtisha kwa kumwonya kuwa tume ya KRA itamwandama.

Seneta huyo wa ANC alisema kuwa mrengo unaounga mkono mfumo wa ugavi wa fedha uliopendekezwa na Kamati ya Fedha ulikuwa ukidhani kuwa anadaiwa Sh8 milioni na KRA, madai ambayo alishikilia kuwa ni ya uongo.

Mnamo Alhamisi ilidaiwa kuwa maseneta wengine wanaopinga mfumo huo unaopendelewa na serikali walipokea vitisho. Nao ni Naibu Kiranja wa Wengi Farhiya Ali, Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Mithika Linturi (Meru) na Seneta wa Machakos Boniface Kabaka.

Mnamo Ijumaa Bw Murkomen na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja walimshutumu Spika wa Seneti Ken Lusaka kwa kupendelea mrengo unaounga mkono mfumo unaopendelewa na Serikali.

Walidai kuwa Bw Lusaka amekuwa akifanya mikutano na maseneta hao kuwarai washinikize kuahirishwa kwa kikao cha seneti kwa mara nyingine mnamo Jumatatu

“Tafadhali refarii; koma kutoa mafunzo kwa timu moja. Turuhusu sote tukutane uwanjani,” Bw Sakaja akasema kupitia Twitter.

Kikao cha Jumatatu ni cha tisa katika msururu wa vikao vya Seneti ambavyo vimeandaliwa kujaribu kusaka makubaliano kuhusu suala hilo.