NA SAMMY WAWERU
KATIBU Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala ametishia kuvamia makazi ya kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), endapo Jumatatu ataelekeza maandamano Ikulu Nairobi.
Bw Malala alisema kwamba hatua hiyo itasaidia kuzima njama ya maandamano ya upinzani.
Kinara wa Azimio la Umoja – One Kenya, ambaye pia ni kiongozi wa ODM, Raila Odinga ametangaza kuwa maandamano ya Jumatatu, atayaelekeza katika Ikulu ya Rais akitumia msingi wa kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha inayozidi kulemea Wakenya.
Malala alisema ataongoza mwenyewe vuguvugu la wafuasi wa UDA kuvamia nyumbani Karen kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Katibu Malala alitoa tishio hilo wakati akizungumza katika Chuo Kikuu cha Machakos, katika kongamano la chama hicho kuhamasisha wajumbe kuhusu uchaguzi wa mashinani wa chama unaotarajiwa kufanyika.
“Wewe Raila tunakuambia, kwa sababu umesema utaelekeza maandamano Ikulu, mimi kama katibu mkuu nitaongoza wafuasi wa chama chetu kupeleka maandamano nyumbani kwako Karen utakapokuwa ukisumbua rais,” akasema.
Ida aandae chai na ugali
Malala vilevile alimtaka mke wa Raila, Bi Ida Odinga kuandalia waandamanaji watakaokita kambi kwake chai na ushumbi wa ugali.
“Pia, tunaambia Ida Odinga aandae chai na ugali. Endapo unadhani (akielekeza matamshi kwa Raila Odinga) una watu, utajua serikali ina watu wengi kuliko wewe,” alisema.
Huku Ikulu ya Rais Nairobi ikiwa chini ya ulinzi mkali, Bw Malala alisema maandamano ya UDA Karen kwa kiongozi wa ODM yatakuwa ya amani.
“Ajiandae, na ajue kwamba Ikulu ina maafisa wa GSU, Recce na wa kijeshi. Raila, una nini katika makazi yako?” akahoji, akishauri wakazi wa Machakos kutoshiriki maandamano.
Raila Odinga na vinara wenza Azimio wamekuwa wakiikosoa serikali tawala ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt William Ruto, wakisema si halali, licha ya mahakama ya upeo kuharamisha kesi ya Raila kupinga matokeo ya kura ya urais Agosti 9, 2022.
Rais Ruto ameonya upinzani, akisema endapo maandamano yao yatavuruga amani serikali haitakuwa na budi ila kukabiliana nao kisheria.