Malala amtaka Rais kuadhibu wanaomsumbua chamani

Malala amtaka Rais kuadhibu wanaomsumbua chamani

Na SAMMY WAWERU

Seneta wa Kakamega Bw Cleophas Malala amemhimiza Rais Uhuru Kenyatta kuelekeza mjeledi kwa viongozi na wanasiasa wanaomtatiza katika chama tawala cha Jubilee, akidai wanamzuia kuafikia ahadi zake kwa wananchi.

Akisifia vinara wa National Super Alliance (Nasa), , kuunga mkono salamu za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Bw Malala alisema hatua hiyo imechangia kusheheni kwa amani nchini.

Bw Raila Odinga ndiye kiongozi wa Nasa. Wengine ni Mabw Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Isaac Ruto wa Chama Cha Mashinani.

“Kabla ya Handisheki, tuliishi kuandamana na kuhangaishwa na gesi ya vitoa machozi. Viongozi wote wa Nasa wameunga mkono salamu za maridhiano kati yako Rais na Raila Odinga…ila katika mrengo wako, Jubilee (JP) kuna shida,” akasema seneta huyo mnamo Jumamosi wakati wa hafla ya mazishi ya Hannah Atsianzale, mamake Musalia Mudavadi.

“Rais ninakuomba ulainishe upande wako, una watu wanaokusumbua kiasi cha kushindwa kutekeleza ajenda na ahadi zako kwa wananchi. Chukua rungu nyorosha watu wanaokukosea heshima,” seneta huyo akahimiza Rais Kenyatta ambaye pia alihudhuria mazishi ya Mama Atsianzale yaliyofanyika eneo la Mululu, Kaunti ya Vihiga.

Kauli ya Malala imejiri siku moja baada ya wandani wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto na ambaye amekuwa mkosoaji wa azma ya Handisheki na Ripoti ya Maridhiano (BBI), kuweka wazi kuhusu chama kipya cha UDA kinachohusishwa naye.

Mwaka uliopita, 2020 wandani wa Dkt Ruto walioshikilia nyadhifa mbalimbali bunge la seneti na kitaifa walibanduliwa, mchakato uliotafsiriwa na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa kama njiamojawapo kujaribu kuzima ndoto za Naibu Rais kuingia Ikulu 2022.

You can share this post!

Kenya Morans kuingia kambini Januari 11 kwa mechi za kufuzu...

Mwanaume akata mkewe miguu kwa kumtoroka