Malala na Echesa mafichoni wakisakwa na polisi kwa kuzua vurugu Matungu

Malala na Echesa mafichoni wakisakwa na polisi kwa kuzua vurugu Matungu

Na SAMMY WAWERU

SENETA wa Kakamega Bw Cleophas Malala na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa wanasakwa na maafisa wa polisi kwa madai ya kuchochea vurugu na fujo katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Matungu uliofanyika Alhamisi.

Hali tete ilishuhudiwa mchana kutwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, wanasiasa hao walipowasili kufuatilia shughuli za uchaguzi.

Katika kituo cha Shule ya Msingi ya Bulonga, Matungu wakati shughuli za kupiga kura zikiendelea, Bw Echesa alinaswa akimzaba kofi afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Waziri huyo wa zamani aliskika akitaka kuelezwa kwa nini maajenti wa chama cha UDA na ambacho kinahusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, walifurushwa kituoni.

Ni tukio lililokashifiwa na IEBC, Mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati akiisihi idara ya polisi kumtia Echesa nguvuni.

“Uvamizi huo ni hatia, na ninaihimiza idara ya polisi kumkamata mhusika, achukuliwe hatua kisheria,” Bw Chebukati akaambia wanahabari baada ya kuzuru kituo cha kupigia kura cha Kiwanja Ndege, Naivasha, ambapo pia uchaguzi mdogo wa udiwani ulikuwa ukiendelea.

Naye seneta Malala, aliibua malalamishi dhidi ya chama cha ODM na ambacho kinaongozwa na Bw Raila Odinga, kwamba kilisakata njama ya wizi wa kura ili mgombea wa chama hicho, Paul Were atwae ubunge wa Matungu.

Wawaniaji wengine wenye ushidani mkali katika kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Mabw Oscar Nabulindo (ANC) na Alex Lanya (UDA).

Malala amesisitiza kwamba chama cha ANC na ambacho kinaongozwa na Bw Musalia Muvadadi hakitakubali matokeo ya uchaguzi huo mdogo, kwa kile alisisitiza zoezi la upigaji kura katika vituo 20 lilikumbwa na udanganyifu.

Vurugu na fujo za mchana kutwa zinasemekana kusababisha baadhi ya watu kujeruhiwa.

Ni matukio ambayo yamesababisha seneta Malala na Echesa kuenda mafichoni, baada ya kugundua wanasakwa na maafisa wa polisi.

Maafisa wa usalama wanaendelea kushika doria katika makazi ya Echesa yaliyoko eneo la Shibale, Mumias ya Kati, Kaunti ya Kakamega, wakimtafuta waziri huyo wa zamani.

Duru zinaarifu wabunge kadha walikamatwa Matungu kutokana madai ya kuhonga wapigakura.

You can share this post!

Mlinzi wa Malala akamatwa kwa kufyatua risasi hewani

Raila njiapanda Pwani ikijitafutia ‘mkombozi’ mpya