Malalamiko tele chombo cha kukagua mizigo kikiharibika katika uwanja wa ndege wa Manda

Na KALUME KAZUNGU

WASAFIRI wa ndege wanaotumia uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu wameisuta Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) kwa kuchelewa kurekebisha mashine ya kukagua mizigo na abiria kwenye uwanja huo.

Mashine hiyo ilileta hitilafu na kusita kufanya kazi karibu wiki mbili zilizopita, hali iliyolazimu maafisa wa usalama kufanya upekuzi kwa mikono.

Mashine iliyoharibika hupekua mizigo na abiria kupitia mfumo wa X-Ray, ambapo hakuna haja ya abiria au mizigo kushikwa na wahudumu wa viwanja vya ndege.

Wasafiri walisema mbali na kuhatarishwa kuambukizwa Covid-19, mfumo huo wa upekuzi wa moja kwa moja pia umekuwa ukiwapotezea muda mwingi kando na kuwa hauna hakikisho la kiusalama.

Bi Fatma Athman ambaye ni msafiri wa mara kwa mara kupitia uwanja wa ndege wa Manda alisema mara nyingi amelazimika kuunga foleni na mizigo yake akisubiri kukaguliwa, hali ambayo ni kinyume wakati mashine ya X-ray inapofnya kazi.

“Sipendelei hali ilivyo sasa. Warekebisha mashine yao ya kukagua abiria na mizigo,” akasema Bi Athman.

Msafiri mwingine, Bw Mohamed Omar, alilalamika kuwa mbinu ya kutumia mikono kwa upekuzi si salama kwani huenda ikatumiwa na wakora kuendeleza maovu yao.

“Mashine ya X-ray ndiyo mwafaka kwa shughuli hii ya upekuzi. Yanayofanyika yanahatarisha maisha yetu,” akasema Bw Omar.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa KAA Ukanda wa Pwani, Bw Peter Wafula alisema mashine ya X-Ray inayokagua mizigo pekee ndiyo ilileta hitilafu na tayari imerekebishwa.

“Tuligundua kuwa ukanda wake ulikuwa umeraruka. Tayari tumeushona na mashine inafanya kazi. Pia tumeagiza ukanda tofauti kutoka Malindi kufikishwa uwanja wa ndege wa Manda ili kurekebisha tatizo hilo kwa njia ya kudumu. Hakuna la kuhofia kwa sasa,” akasema Bw Wafula.