Makala

Malalamiko ya mifugo wakaidi

February 25th, 2024 1 min read

NA RICHARD MAOSI

MAMA mboga kutoka mjini Naivasha na Gilgil, wameripoti kuhangaishwa na mbuzi, kondoo na ng’ombe wanaozurura sokoni bila wenyewe.

Ni hali ambayo imewafanya wengi wao kukadiria hasara, hasa pale mifugo wanapovamia vibanda vyenye mboga na matunda.

Wanalalamikia kero hii, ambapo wanalazimika kukimbizana na wanyama hao wakorofi wakisaka malisho.

Wanashutumu wenye mifugo hao wakipendekeza wachukuliwe hatua kali, na Maafisa wanaotoa Huduma ya Afya kwa Umma.

Bi Alice Kangema mkaazi wa Karagita anasema mji wa Naivasha umepoteza uzuri wake wa hapo awali, maana utawakuta mbwa na paka wakimenyana karibu na biashara za watu.

“Isitoshe, wakati mwingine mbwa huhatarisha maisha ya wanafunzi wanaorauka kwenda shuleni asubuhi na mapema,” Alice akaambia Taifa Leo Dijitali.

Alisema hata ingawa baadhi ya wamiliki wa mifugo wamepewa onyo kali, bado mbuzi, kondoo na ng’ombe wanaishi barabarani.

Cha kushangaza ni kwamba wenyewe hawajulikani.

Akielezea kukerwa kwake na tabia za wanyama hao wa nyumbani, Grace Gateh alisema endapo hawana wamiliki “huenda basi wakawa ni majini”.

“Ukijaribu kuiba au kuchinja mmoja ndio utajua wenyewe ni kina nani,” kasema.

Alifichulia Taifa Leo Dijitali kuwa wenye mifugo hao huwa hawajulikani, ila hutokea ghafla pale mbuzi au ngombe wao wanapokumbwa na hatari.

Isaac Kakoginih mkaazi wa Mombasa anaungama kwamba visa kama hivi vimejaa katika Kivukio cha Likoni.

Anasema mbuzi na ngombe wana ujuzi wa kuvuka kwa kutumia feri kutoka ng’ambo moja hadi nyingine.

Cha kusataajabisha ni jinsi wamemudu kujipatia ujuzi wa kutumia kivukio bila kuelekezwa na binadamu.