Malalamiko ya Nigeria yasababisha mashindano ya handiboli kuahirishwa

Malalamiko ya Nigeria yasababisha mashindano ya handiboli kuahirishwa

Na AGNES MAKHANDIA

MAKALA ya 25 ya Kombe la Afrika la handiboli la wanaume yameahirishwa kutoka Januari 15-23 hadi Juni 22-Julai 2 nchini Morocco na droo kufutiliwa mbali.

Inasemekana Shirikisho la Handiboli Afrika (CAHB) limechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa Nigeria ambayo haikuridhishwa na droo ya mashindano hayo.

Katika droo iliyofanywa Desemba 2021 nchini Morocco, timu ya Nigeria ilitiwa katika Kundi B pamoja na Kenya na mabingwa watetezi Angola. Kundi A lilikuwa na Misri, DR Congo, Gabon na Cameroon nazo Tunisia, Cape Verde, Guinea na Senegal zilitiwa katika Kundi C.

CAHB limesema droo mpya itafanywa Juni.

Wakati huo huo, Shirikisho la Handiboli Kenya (KHF) limetangaza droo ya kipute cha Super Cup kitakachoandaliwa Machi 5-6 na Machi 12-13.

Kipute hicho huhusisha klabu zilizokamilisha Ligi Kuu katika nafasi sita za kwanza kwa upande wa wanaume, huku shindano la kinadada likikutanisha timu nne za kwanza.

Wafalme Cereals Board (NCPB) wako katika Kundi A pamoja na Black Mamba na majeshi (KDF).

Chuo Kikuu cha Strathmore, ambacho kilimaliza ligi nambari mbili, kimetiwa katika Kundi B linalojumuisha pia maafisa wa usalama wa GSU pamoja na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Shindano la kinadada litatumia mfumo wa mzunguko likihusisha Nairobi Water (mabingwa), KDF, NCPB na Nanyuki.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Bingwa wa marathon Chepng’etich kivutio Nairobi Cross...

Pigo kwa Obado korti ikikataa kesi dhidi yake kusikilizwa...

T L