Malalamiko ya wabunge baada ya SRC kupunguza mapato yao

Malalamiko ya wabunge baada ya SRC kupunguza mapato yao

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wamelalamikia hatua ya Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC) kuondoa au kupunguza marupurupu ambayo wamekuwa wakipokea.

Aidha, wamekerwa na hatua ya tume hiyo kukataa pendekezo lao la kutaka mshahara wao ungezwe hadi Sh1.2 milioni kwa wiki na wawe wakilipwa marurupuru ya nyumba, sawa na majaji.

Mishahara ya wabunge na maseneta itasalia Sh710,000 kila mmoja kila mwezi, katika bunge la 13, litakaloanza vikao Septemba 2022. Hii ni baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Katika ripoti yake ambayo ilitolewa kwa vyombo vya habari wiki hii, SRC imeondoa marupurupu ya Sh5,000 ambayo wabunge na maseneta hulipwa kwa kuhudhuria kila kikao.

Bunge la kitaifa hufanya vikao vine kila wiki ilhali seneti hufanya vikao vitatu kila wiki.

Kwa kuwa kuna jumla ya wabunge 349 na maseneta 67, kuondolewa kwa marupurupu ya vikao kutaifanya serikali kuokoa Sh382.2 milioni kila mwaka. Hii ni endapo hatua ya SRC itatekelezwa katika Bunge la 13 linaloanza Septemba mwaka huu.

Aidha, tume hiyo imepunguza marupurupu yao ya usafiri kutoka Sh187 hadi Sh112 kwa kila kilomita ambayo wabunge husafiri kutoka majengo ya bunge hadi maeneo bunge yao.

Hata hivyo, marupurupu ya vikao vya kamati yamedumishwa. Kulingana na viwango vya sasa, mwenyekiti wa kamati ya bunge hupokea Sh10,000, naibu wake hupokea Sh7,5000 na wanachama wa kamati hutia kibindoni Sh5,000 kwa kila kikao.

Hata hivyo, SRC imeshikilia kuwa vikao vya kamati havifai kuzidi vinane kila mwezi.

Wakati huu, kamati za bunge zinafanya zaidi ya vikao hivyo kila mwezi, hali ambayo huimarisha mapato ya wabunge.

Wabunge waliozungumza baada ya mkutano wao usio rasmi (Kamukunji) mnamo Jumatano, walisema sio haki kwa SRC kuondoa marupurupu wanayolipwa kwa kuhudhuria vikao vya bunge na kupunguza marupurupu ya usafiri.

“Hii tume ya SRC inataka kutufanya tuwe fukara kwa kupunguza mapato yetu. Wasiporejesha marupurupu yetu nasi tutapunguza bajeti yao kwani tuko na uwezo wa kufanya hivyo,” akasema mbunge mmoja aliyeomba tulibane jina lake.

“Hao makamishna wa SRC hupokea mishahara kamili kama wafanyakazi wa kawaida ilhali hawafanyi kazi kila siku. Wao hupata marupurupu ya vikao na marupurupu ya nyumba lakini wanatunyima marupurupu ya nyumba,” akaongeza Mbunge.

Mbunge mwingine kutoka Rift Valley alipendekeza kuwa tume hiyo inafaa kuvunjiliwa mbali kwa sababu imevuka mipaka katika utendakazi wake.

“Wajibu wa SRC ni kutoa ushauri kwa asasi mbalimbali kuhusu suala zima la mishahara na marupurupu. Haina mamlaka ya kuondoa marupurupu au mishahara ambayo maafisa wa serikali hupokea. Huo ni wajibu wa tume husika. Hapa bungeni, Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ndio ina mamlaka ya kuongeza au kupunguza mishahara na marupurupu ya wafanyakazi kulingana na bajeti yake,” akaongeza.

Wabunge walijulishwa kuhusu hatua hiyo ya SRC wakati wa Kamukunji hiyo iliyoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi katika majengo ya bunge, Nairobi.

Bw Muturi ndiye Mwenyekiti wa PAC ambayo ndio hulisha mishahara na marupurupu ya wabunge, maseneta na wafanyakazi wote wa asasi ya bunge (Bunge la Kitaifa na Seneti).

Hata hivyo, wabunge na maseneta watapokea ruzuku ya Sh7.55 milioni za kununua gari yenye ukubwa wa injini usiozidi 3000cc.

Spika Muturi pia ameisuta SRC kwa kile alichotaja kama kutozingatia haki inakadiria mishahara na marupurupu ya wabunge.

Ingawa katiba inawaorodhesha wabunge miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali, sawa na mawaziri na majaji, wabunge hawajafaidi sawa na maafisa hawa.

Mr Muturi said that whereas the constitution categorises “Wabunge ndio maafisa wa serikali ambao hawana marupurupu ya nyumba, ilhali wako na vituo viwili vya kufanyakazi; majengo ya bunge na maeneo bunge yao.

Hatua ya SRC kuondoa marupurupu ya vikao itachangia idadi ndogo ya wabunge kuhudhuria vikao na hivyo itakuwa vigumu kwa ajenda za serikali kuu kupitishwa,” akasema Bw Muturi.

“Kuna wabunge ambao wameniambia kwamba ikiwa watachaguliwa tena watakuwa wakija bungeni kujiandikisha kuwa wamefika kisha wanaondoka,” akaongeza.

Mawaziri na Majaji hupata marupurupu ya nyumba ya Sh400,000.

Zaidi ya hayo mawaziri, majaji na makatibu wa wizara hupokea Sh7 milioni kama marupurupu ya kununua magari. Vile vile, hupewa gari la serikali ambalo mafuta yake hugharamiwa na mlipa ushuru.

“SRC inawatesa wabunge bila sababu, ilhali wenzao kote duniani na hata mataifa jirani hawatendewi hivyo,” Bw Muturi akalalamika.

Kando na ruzuku ya kununua magari wabunge pia hupokea Sh356,525, kila mwezi za kutunza magari.

Wao pia wana bima ya matibabu ya Sh10 milioni ya kugharamia kulazwa hospitalini, bima ya Sh300,000 kugharamia matibabu ya kurudi nyumbani, Sh150,000 ya kujifungua na Sh75,000 ya utunzaji meno.

Serikali inalenga kupunguza mzigo wa ulipaji mishahara ya walimu ambao unazidi kuongezeka kila mwaka. Kiasi kikubwa cha mapato ya serikali hutumika kulipa mishahara na hivyo kuacha pesa kidogo za kufadhili miradi ya maendeleo.

Kuepuka makabiliano

Ili kuzuia makabiliano na wabunge, SRC itachapisha mabadiliko hayo katika gazeti rasmi la serikali baada ya bunge kusitisha vikao vyake mnamo Juni 9, 2022 kutoa nafasi kwa uchaguzi mkuu.

Mnamo 2017, SRC ilichapisha ratiba ya mapunguzo ya mishahara ya maafisa wakuu wa serikali, akiwemo rais n wabunge, mnamo Julai 10, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8.

Uaumuzi wa kupunguza mapato ya wabunge unajiri baada ya makubaliano ambayo serikali iliweka na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kwamba nyongeza za mishahara ya watumishi wa umma zisitishwe kwa miaka miwili hadi 2025.

Hatua hii inalenga kuiwezesha serikali kupata pesa za kufadhili miradi kama vile ujenzi wa barabara na hivyo kubuni nafasi za ajira.

SRC inasema kuwa mzigo wa mishahara katika sekta ya umma ulifika Sh827 bilioni kufikia Juni 2020 kutoka Sh615 bilioni mnamo 2016. Hii ni sawa na ongezeko la kiwango cha asilimia 34.

  • Tags

You can share this post!

Kocha McCrath kutegemea ujuzi wake kuvumisha Kenya Sevens

Bei ya mafuta yapanda tena

T L