Siasa

Malalamishi 10 ya Mlima Kenya kwa Rais Ruto

June 2nd, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya wanasiasa na wenyeji wa Mlima Kenya sasa wasema wana malalamishi yanayofika 10, wakimtaka Rais William Ruto kulainisha hali na anapokemea siasa za ukabila, mambo hayo yapewe kipaumbele.

Gavana wa zamani wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu anakiri ni kweli Mlima Kenya walimchagua Dkt Ruto kuwa Rais katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Yeye binafsi anasema kwamba amekuja kujutia kuwa mmoja wa waliowarai wenyeji kumpigia Dkt Ruto kura, suala la kama yeye binafsi ni mfaafu kutangaza hayo likijitokeza ikizingatiwa ameshtakiwa mahakamani kwa madai kwamba, akishirikiana na wandani wa familia yake, alifisadi takriban Sh558 milioni.

Bw Waititu aling’atuliwa na Bunge la Kaunti ya Kiambu na baada ya Dkt Ruto kuwa Rais, alimteua kuwa mwenyekiti wa bodi ya usafishaji Mto Nairobi.

Lakini mahakama ikaamua baada ya kesi kuwasilishwa, kwamba aliyekuwa ameng’atuliwa mamlakani hakuwa na ufaafu wa kupewa kazi ya umma.

“Mimi naomba wenyeji wa Mlima Kenya msamaha kwa kuwa niliwarai kuchagua serikali ya Kenya Kwanza. Hali imeishia kuwa ya ningalijua singalifanya hivyo,” Waititu akasema.

Lisilofichika ni kwamba kwa sasa mjadala kuhusu ufaafu wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais Ruto kwa masilahi ya wenyeji limezuka, iwe ni kutoka kwa kinywa cha Bw Waititu au kwa vinywa vya wengine katika gumzo za majukwaa mbalimbali mashinani.

Kufikia sasa, wanaoisuta serikali ya Kenya Kwanza kwa kile wanadai ni baadhi ya wanasiasa ndani yake kufadhili njama ya kumdunisha Naibu Rais Rigathi Gachagua miongoni mwa masuala mengine tisa.

Hii hujuma wanadai ni ya kuzima mjadala wa ugavi wa mamlaka na rasilimali za nchi kwa kuzingatia idadi ya watu. Hivyo katika orodha suala la ugavi wa rasilimali ni malalamishi pia.

Suala jingine ni kukumbatia kinara wa upinzani Bw Raila Odinga.

Vilevile, walalamishi wanadai kuna njama ya kumfikia Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pasipo kumhusisha Bw Gachagua.

Malalamishi mengine ni kuhusu kuliinua kanisa la Kipentekosto (AIPCA) kuliko mengine, kuzembea katika kulainisha bei za bidhaa za kilimo, kuhadaa waagizaji bidhaa wa Nyamakima jijini Nairobi kwamba serikali ingewapunguzia gharama za kibiashara, na pia kuwaacha kwa mataa baadhi ya waliomsaidia Rais kuingia ikulu.

Pia, baadhi ya wandani wa kiongozi wa nchi wamesutwa kwa kujaribu kunyapara siasa za Mlima Kenya.

Tayari, Bw Gachagua na Mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya wameripoti hadharani kwamba “baadhi ya wanasiasa walio karibu na Rais wameingiwa na kiburi kiasi cha kufadhili misukosuko ya kisiasa katika kaunti nyingi za Mlima Kenya.

“Kuna wachache wanaomzingira Rais ambao wameingiwa na kiburi na ndio hao wanatuletea matatizo eneo hili letu la Mlima Kenya,” akasema Gachagua huku naye Bw Gakuya akisema kwamba “njama za misukosuko hapa kwetu zinasukwa kutoka Rift Valley”.

Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Bw Jeremiah Kioni naye kwa shtaka la pili anasema kwamba utawala wa Rais Ruto ni janga kwa wenyeji wa Mlima Kenya “kwa kuwa sisi anatunyima haki yetu ya rasilimali na uwakilishi kwa kuzima mjadala wa ‘mtu mmoja, shilingi moja’ uwe sheria.

Bw Waititu ndiye mmiliki wa mashtaka matatu ambayo ni kuacha kwa mataa washirika wake waliompambania, kukumbatia Bw Odinga na pia kusaka ushirika wa Bw Kenyatta.

“Tuliambiwa na Dkt Ruto kwamba sote tiliokuwa tumewekelewa kesi kutokana na misimamo yetu ya kisiasa kwamba tungesaidiwa kuoshwa dhambi hizo za kubandikwa. Mimi ni mfano wa walioachwa kwa mataa,” akadai Bw Waititu.

Bw Waititu anaongeza kwamba Rais Ruto amesahau kwamba alichaguliwa kwa wingi wa kura za Mlima Kenya kama ukaidi dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga.

“Huku akifahamu vyema eneo hili lilikuwa limekataa ushirika na Bw Odinga, Rais Ruto alitudhihaki kwa kumkumbatia na kumfanya mmoja wa wandani wa serikali kiasi hata cha kuzuru taifa la Uganda wakiwa pamoja,” akasema Bw Waititu.

Bw Waititu aliongeza kwamba shtaka la tano ni kuhusu dokezi kwamba “Rais Ruto pia anamsaka Bw Kenyatta waridhiane na washirikiane ikifahamika vyema kwamba akifanya hivyo nje ya kushirikisha Bw Gachagua, atakuwa amechochea utengano wa wenyeji”.

Sita, mwenyekiti wa muungano wa madhehebu asili ya Mlima Kenya, Askofu Edward Nyutu anahisi Rais Ruto na Bw Gachagua wakiwamegea minofu viongozi wa dini, wagawanye kwa makanisa na madhehebu mbalimbali kwa usawa.

Kinara wa Narc Kenya Bi Martha Karua anasema kwamba serikali ya Ruto licha ya kuwaahidi wakulima bei bora za bidhaa za kilimo, hali ni bado.

“Huku tukiwa na msemo kwamba mkono wa mkulima hauvunjwi, utawala huu unavunja mkono huo na pia mgongo. Hali katika sekta ya kilimo bado ni Ile ya utumwa,” akasema Bi Karua.

Suala la nane dhidi ya Rais Ruto ni ushuru unaosemwa kuwa wa kiholela. Aliyekuwa mwaniaji wa urais mwaka wa 2013 Bw Peter Kenneth anasema kwamba “ushuru wa Rais Ruto ndio utamng’oa mamlakani mwaka 2027”.

Anasema kwamba Mswada wa Fedha wa 2023 uliishia kuwa janga “huu nao unaopendekezwa wa 2024 ukiwa hatari zaidi kwa uwekezaji kutokana na viwango vipya vya kodi za lazima”.

Aliyekuwa Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara za Elimu na Spoti Bw Zack Kinuthia anasema kwamba utawala wa Rais Ruto umehadaa wawekezaji wa Nyamakima “kwa kuwa licha ya kuwaahidi gharama za chini za kibiashara na pia sera za kuwakinga kutokana na ushindani wa wawekezaji wa kigeni, alisahau au alipuuza”.

Anasema kwamba ushuru wa uagizaji bidhaa bado uko juu na wawekezaji wa kigeni bado wanatawala safu za kibiashara.

Suala la 10 linatoka kwake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu Wachira wa Kiago ambaye analalama kwamba kuna wandani wa Rais Ruto ambao wamejitwika jukumu la kunyapara hata utamaduni wa wenyeji wa Mlima Kenya.

“Tunawasikia wakitusuta kwamba tuko na ukabila wakituona tumekutana kusemezana kuhusu yanayotuhusu. Sisi hatuwakazii kwa kufuatilia mikutano au hafla zao,” akasema Bw Wa Kiago.

[email protected]