Makala

MALENGA WA WIKI: Kifo cha Sudi Kigamba ni pigo kwa tasnia ya ushairi na taaluma ya Kiswahili

December 6th, 2020 2 min read

Na HASSAN MUCHAI

MAREHEMU Al- Haji Sudi Kigamba aliyejulikana kwa lakabu ya ‘’Mwanamrima’’ alikuwa na mambo mawili aliyotaka kutimiza pindi angetua nchini Kenya mwezi Machi au Aprili mwaka 2021.

Kupitia ujumbe wake ulionukuliwa Agosti 16, 2019, Marehemu alitaka kuyakusanya mashairi ya marehemu Mwalim Mbega akiwa na nia ya kuandika wasifu wake.

Kilichomkwaza sana kutimiza azma hii ni kuwa, kuna watu waliokuwa na maelezo hayo nchini Uholanzi na Ujerumani ila hakuwa na uwezo wa kuwafikia. Akiwa na nia hiyo ya kuandika wasifu, Marehemu Sudi alikuwa pia akinuia kutimiza azma ya babake na kutoa Diwani ya “Akina Mwakamadhy’’.

Aliwahi kusema ‘’Inshallah yule mama ameniita kupata historia na picha zake lakini alizitoa kwa mama Joyce wa Netherlands. Nataraji kukaa kwake kwa siku tano halafu nikaje Dar kwa mwanawe wa kike kwanza.’’

Hata hivyo, alijua kibarua kilichokuwa mbele yake kingekuwa kigumu ikizingatiwa kazi na miswada mingi ya marehemu Mbega imepotea.

Pili, watunzi wakongwe ambao angewategemea kwenye mahojiano tayari wameaga dunia. Hata Tanga alikoinukia alijua kuwa wazee hao hawako.

Tatu, Kigamba alikuwa na matarajio ya kufika Kijiji cha EkalaKala tarafa ya Matuu, Kaunti ya Machakos alikozikwa mlezi wake wa ushairi marehemu Mwalim Mbega ili kumfanyia dua ya hitIma. Hitima au Khitima ni dua anayoombewa aliyekufa kwa kumtakia rehema na radhi za Mwenyezi Mungu.

“Naam, tumepanga na watoto wake tukamfanyie hitima. Sasa nakusanya senti Inshallah mwezi wa tatu au wa nne si mbali,” aliwahi kusema.

Kifo cha ghafla cha Sudi Kigamba kimeingia wakati mchango wake katika fani ya ushairi na lugha ya Kiswahili ulikuwa ukihitajika sana.

Kigamba aliaga dunia Novemba 25 kwa kile kinachoaminika kuwa mshtuko wa moyo. Cha kushangaza ni kuwa, Kigamba ameaga dunia mwezi sawa na mlezi wake wa lugha Mwalim Mbega aliyefariki Novemba 2007.

Marehemu alikuwa amejihusisha na makundi mengi ya kijamii alikotegemewa kufafanua usuli wa matumizi ya misamiati mingi ya Kiswahili.

Mawasiliano yake ya mwisho na kundi la Kiswahili na Ushairi yalikuwa mwezi jana siku chache kabla ya kuaga dunia alipochangia rai yake kuhusu matumizi ya neno Kisogo/Kishogo.

Hakuna aliyetarajia kuwa kifo chake kingetokea ghafla na kukatiza matumaini yake sawa na wapenzi wa mashairi.

Mnamo Novemba 14, 2020, alisema, “Hapa pagumu ustadhi maana pia kuna uchogo na kichogo hata shogo lakini naona Sheikh Mbega alimdhihaki mshairi aliyesema shogo. Mimi nafikiri ni lahaja tu zinakinzana na hilo si jambo kubwa sana; zote ziko sawa chambilecho wajuzi. Niko mbali ningekwenda kupekua maakaba zangu nilizo nazo inshallah tujaribu siku nyingine.’’

Mbali na fafanuzi hizo, Kigamba alikuwa mshairi shupavu na alitumia muda mwingi kuchangia mada mbalimbali zilizotolewa na walumbi wenzake. Itakumbukwa kwamba alikuwa muasisi wa malumbano ya Mbega na Chombo mwaka 1993 kuhusu mwanaharamu.

Mrahano huo ulichukua zaidi ya miaka saba ulipokamilika mwaka 1997!

Baada ya kupokea habari za kifo chake, watunzi wa mashairi na watetezi wa lugha ya Kiswahili walituma jumbe zao za kuomboleza kifo hiki kwa namna wanayoijua na kuipenda wenyewe- ushairi.

Kati ya waliotuma risala zao ni Shaha Rajab Pilau, Abdallah Omar -Chetezo, Juma Salim Makayamba, Juma Shumbana, Hassan Morowa, Yitzaq Mwago, Kazungu Samuel, Mzee Thomas Koskei, Elvis Kosgey, Ludovick Mbogholi na wengineo.

Hadi tulipokuwa tukiandaa makala haya, matayarisho ya kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka jijini London, Uingereza ili kuzikwa nyumbani Tanga yalikuwa yakiendelea.

Jumapili ijayo tutaangazia jinsi Kigamba alivyopandisha mori washairi wa Kenya mwaka 1993 kwa kuzua mrahano mkali baina ya Mbega na Chombo.