MALENGA WA WIKI: Kutana na Juma Mrisho ‘Ustadhi Chapuo’ aliyekuwa mwiba wa kulumbana

MALENGA WA WIKI: Kutana na Juma Mrisho ‘Ustadhi Chapuo’ aliyekuwa mwiba wa kulumbana

Na HASSAN MUCHAI

Kiokotwe kaokotwa, kiokotwa cha thamani,

Kwapani kakifumbata, hali yake afueni,

Kiokotwa kinameta, chavutia wapembeni,

Kiokote kaokotwa, majungu kwake ya nini?

 

Mlicheka aokota, hana kazi asilani,

Jaani anamo pita, huingia uchafuni,

Riziki akitafuta, mkono wende kinywani,

Kiokote kaokotwa, majungu kwake ya nini?

 

Mavumbi kimemfuta, uchafu hauuoni,

Kiokote ananata, neema imebaini,

Kukosa sio kupata, aitwa bwana fatani,

Kiokote kiokotwa, majungu kwake ya nini?

Juma Mrisho ‘Chapuo’

Juma Mrisho Hamsini Watuta anayejulikana kishairi kama ‘Chapuo’, si mgeni kwa macho ya wapenzi wa mashairi.

Mrisho ni mshairi na mwandishi hodari wa tamthilia, wa miaka mingi, elimu aliyoipata kutoka kwa watunzi wa kale kama vile Mathias Mnyampala.

Mshairi huyu ambaye makazi yake kwa sasa ni Dare -es -Salaam, Tanzania, alizaliwa mwaka 1946 mjini Dodoma na kupata masomo yake katika shule ya msingi ya Dodoma Middle kuko huko Tanzania, alilazimika kuyakatiza akiwa katika darasa la nane kutokana na sababu ambazo hangeweza kuziepuka.

Alijiunga na chuo kimoja kwa elimu ya uhandisi wa umeme kabla ya kuajiriwa na shirika la reli la Tanzania hadi mwaka 1975 alipostaafu na kuingilia shughuli za kibnafsi. Hapa ndipo alipojingiza kikamilifu kwenye sanaa ya uigizaji na sarakasi.

Ni akiwa kijijini hapo Bashirodi, Dodoma alipokutana na washairi wengi waliopenda malumbano. Alivutiwa sana na fani hii na mara moja akaanza kujifunza kuandika beti za mashairi.

Mmoja kati ya washairi waliomvutia Mrisho ni Mnyampala ambaye alipata bahati kukutana naye ana kwa ana.

Mbali na Mnyampala walikuwepo watunzi wengine wenye sifa kubwa kama vile Mahmoud ‘Jitu Kali’, Hamis Amani ‘Nyamaume’’ Makaranga wa Singinda na Hassan Mwalim Mbega wa Kenya miongoni mwa washairi wengine wengi. Mshairi aliyekuwa karibu naye sana ni Mnyampala.

Chapuo anasema siku hizo karibu magazeti yote Tanzania yalikuwa yakifuatilia kwa karibu sokomoko la ulumbi uliokuwa umeibuka baina ya watunzi kutoka Tanga na wale wa Rufiji.

Hapa ndipo alipojuana na marehemu Mbega aliyekuwa amekita kambi kwenye kikosi cha washairi kutoka Tanga.

Mara ya kwanza Mrisho kuingia Kenya ilikuwa mwaka 1969. Alitua mitaa ya Pumwani na Majengo, Nairobi.

Akiwa mitaa hii alibahatika kukutana na wasanii wengine wenye haiba kubwa kama vile marehemu Musa Stephene, Mwalimu Mbega, Abdallah Mwasimba, A A Jino la Simba na wengine wengi.

Musa alikuwa mshiriki mkuu wa mashairi na aliwahi kutoa mchango wake kama mchambuzi wa mashairi kupitia kipindi ‘Nuru ya Ushairi’ kilichokuwa kikisimamiwa na Constancy Mackenzie.

Mrisho anasema maisha yake kishairi yamekuwa na panda-shuka chungu nzima.

Amelumbana na washairi wengi na kujipa ujasiri usio na kifani. Malumbano ambayo angali anayakumbuka ni baina ya Mbega na Chombo kuanzia mwaka 1992 hadi 1998.

‘“Nimeshiriki malumbano mengi sana lakini yaliyoniteka sana ni baina ya Mbega na Chombo. Ingawa ulumbi huu ulikuwa wa kukata na shoka, nasikitika kwamba watunzi waligeuza mada yake na kuleta matusi. Sikufurahia katu,’’ akasema Mrisho kwenye mahojiano ya awali na ukurasa huu.

Akiwa kwenye mrahano huu, Chapuo alitunga mashairi mengi kama vile malumbano si matusi, kutajwa ni sifa, mimi ndiye chapuo na kadhalika.

Itaendelea Jumapili ijayo….

You can share this post!

DINI: Usikate tamaa, kipenga cha mwisho bado

JAMVI: Ushindi wa BBI rungu la kumtwanga Ruto